Rais Bashar al-Assad: Muda si mrefu vita vitamalizika nchini Syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa, muda si mrefu vita ilivyotwishwa nchi hiyo vitamalizika na nchi hiyo kuwa na nafasi kama iliyokuwa nayo hapo awali katika ulimwengu wa Kiarabu.
Rais Assad amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Kuweit la al-Shaahid na kutangaza wazi kwamba, karibuni hivi vita nchini Syria vitafikia tamati na kwamba, kumalizika mgogoro wa nchi hiyo kutaifanya Syria iwe na nafasi yake ile ile iliyokuwa nayo hapo kabla katika ulimwengu wa Kiarabu.
Rais wa Syria ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya vyombo vya habari vya Kiarabu kuwa vibaraka wa asasi za Marekani na za Kizayuni na kubainisha kwamba, hatua ya baadhi ya vyombo hivyo vya habari ya kuanzisha vita vya vyombo vya habari inalenga kuziharibia haiba nchi za Mashariki ya Kati hususan Syria ili wananchi washindwe kuainisha haki katika batili.
Rais Assad ameashiria mafanikio na maendeleo makubwa iliyoyapata Syria katika kukabiliana na magaidi watenda jinai na kusema kuwa, serikali ya Damascus ikiwa na lengo la kukomboa ardhi yote ya nchi hiyo haitalegeza hata kwa futuri moja.
Kadhalika ameashiria kukombolewa sehemu kubwa ya ardhi ya Syria kutoka katika udhibiti wa magaidi na kuwalinda raia mkabala na magaidi matakfiri na kusema kuwa, kuanza mwenendo wa kuikarabati nchi hiyo na kufunguliwa viwanda nchini humo, ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na serikali ya Damascus.