Nov 11, 2018 13:32 UTC
  • Bunge la Iraq lataka kutimuliwa nchini humo askari wa Marekani

Mwanasiasa wa ngazi za juu wa Iraq amesema Bunge la nchi hiyo linatazamiwa kujadili hoja ya kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu huku Baghdad ikiituhumu Washington kuwa inaingilia masuala yake ya ndani.

Ahmad al-Assadi, mbunge wa Muungano wa Ujenzi wa Iraq amesema wabunge wa Iraq wanatazamiwa kuishinikiza serikali iwape ratiba maalumu inayoainisha kufikia lini wanajeshi hao wa Marekani watakuwa wameondoka nchini humo kikamilifu.

Tovuti ya habari ya Arabi21 imemnukuu mbunge huyo akisema kuwa, ingawaje askari wa Marekani walianza kuondoka nchini humo tangu wakati wa bunge lililopita, lakini bunge la sasa linataka kuanishwa muhula wa kundoka kikamiliu nchini humo askari hao vamizi.

Mwanasiasa huyo amebainisha kuwa, baada ya kutokomezwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS), serikali ya Baghdad ina haki ya kuangalia upya suala la uwepo wa askari wa Marekani katika ardhi ya Iraq.

Marekani inatuhumiwa kuunda na kulifadhili kwa hali na mali genge la Daesh (ISIS)

Itakumbukwa kuwa, Marekani iliondoa askari wake kutoka Iraq mwaka 2011. Hata hivyo mwaka 2014 na baada ya kuibuka kundi la ukufurishaji la Daesh, ilitumia kisingizio cha kupambana na kundi hilo na kuanza kurejea tena kijeshi nchini humo kiasi kwamba hivi sasa ina askari wake karibu 5000 ndani ya ardhi ya Iraq.

Mbali na serikali ya Iraq, raia wa nchi hiyo pia wanapinga vikali uwepo wa askari hao wa Marekani ndani ya ardhi ya nchi yao.

Tags