Imarati yafungua upya ubalozi wake nchini Syria baada ya miaka 7
Umoja wa Falme za Kiarabu umefungua tena ubalozi wake katika mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kupita zaidi ya miaka saba tangu ulipoanza mgogoro wa ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Habari ya Syria, shughuli za kuufungua upya ubalozi huo wa Imarati mjini Damascus zimefanyika leo Alkhamisi. Ubalozi huo ulifungwa na Abu Dhabi muda mfupi baada ya kuanza mgogoro wa Syria mwaka 2011.
Huku mgogoro wa kutwishwa Syria ukielekea ukingoni, sanjari na serikali ya Rais Bashar al-Assad na vikosi vyake vikiendelea kudhibiti karibu maeneo yote yaliyokuwa chini ya magenge ya kigaidi, baadhi ya maadui wa Damascus hivi sasa wanaonekana kuanza kubadili msimamo na mtazamo wao kwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Disemba 16, Rais Omar al-Bashir wa Sudan alifanya safari nchini Syria na kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuitembelea nchi hiyo; siku chache baada ya Bunge la Arab League kutaka Syria irejeshwe kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.
Kadhalika Imarati inafungua upya ubalozi wake nchini Syria siku chache baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa majeshi ya nchi hiyo yataondoka katika ardhi ya Syria.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Staffan de Mistura, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria alitoa ripoti yake ya mwisho katika Baraza la Usalama la UN na kutangaza rasmi kufikia tamati majukumu yake nchini Syria.