Vyama vya mrengo wa kulia Israel vinapanga kumuangusha Netanyahu
Baada ya kusambaratika baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel na kuchukuliwa uamuzi wa kufanyika uchaguzi wa bunge wa kabla ya wakati katika utawala huo, vyama vya mrengo wa kulia katika muungano tawala vimekumbwa na mgawanyiko mkubwa na sasa vinafuatilia mpango wa kumuangusha waziri mkuu Benjamin Netanyahu.
Novemba na Disemba 2018 ni miezi iliyotajwa kuwa iliyojaa kiza kwa utawala haramu wa Israel. Awali Israeli ilianzisha vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza na ikashindwa vibaya baada ya siku tatu tu. Kushindwa huko kulipelekea kusambaratika muungano tawala. Nukta muhimu kuhusu kushindwa huko ni kuwa kulithibitisha kuwa, uwezo wa kujihami harakati za muqawama na kupigania ukombozi Palestina ni jambo ambalo limepelekea Israel ishindwe kuendesha vita vya muda mrefu dhidi ya Ghaza. Katika mwaka 2014 vita vya Israel dhidi ya Ghaza viliendelea kwa muda wa siku 51 lakini katika mwezi Novemba mwaka 2018, Israel haikuweza kustahamili vita dhidi ya Ghaza kwa zaidi ya siku tatu.
Disemba mwezi 2018, kulikuwa na jitihada kubwa zilizofanywa na Netanyahu na chama chake cha Likud kwa lengo la kuzuia kusambaratika muungano tawala lakini si tu kuwa jitihada hizo ziligonga mwamba bali hata kulionekana ishara za kugawanyika na kusambaratika mrengo wa kulia wenye misimamo mikali ya kufurutu ada katika utawala bandia wa Israel.
Hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha chini ya miezi minne ijayo, yaani Aprili 9, kutafanyika uchaguzi wa bunge wa kabla ya wakati katika utawala wa Israel. Uchaguzi huo awali ulikuwa umepangwa kufanyika Novemba 2019.
Vyama vya mrengo wa kulia katika utawala wa Israel ndivyo vilivyounda muungano tawala na chama chenye ushawishi mkubwa ni chama cha Likud ambacho kinaongozwa na Netanyahu ambacho kilipata viti vingi zaidi bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Lakini kumeshuhudiwa kudhoofika chama cha Likud na kinara wake, Netanyahu, kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa mara kadhaa na harakati za muqawama, mafaili ya ufisadi ya Netanyahu na mke wake na pia kuongezeka matatizo ya kiuchumi na maisha magumu miongoni mwa Wazayuni.
Netanyahu amekuwa waziri mkuu wa utawala bandia wa Israel tokea Aprili 2009 hadi sasa na ifikapo Aprili 2019 atakuwa madakarani kwa muda wa miaka 10.
Netanyahu anatarajia kuwa, Aprili 9 mwaka 2019 chama chake cha Likud kitapata ushindi kwa mara nyingine na hivyo aendelee kuwa waziri mkuu wa utawala huo haramu. Lakini wakosoaji wake, ikiwa ni pamoja na vyama vya mrengo wa kulia vinataka aondoke madarakani kwani iwapo ataunda baraza la mawaziri kwa mara nyingine huo utakuwa mwisho wa madai ya kuwepo demokrasia katika utawala haramu wa Israel.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Ayelet Shaked waziri wa sheria na Naftali Bennett waziri wa elimu katika baraza la mawaziri la utawala bandia wa Israel na ambao ni kutoka chama cha mrengo wa kulia cha "Nyumba ya Mayahudi" wanakaribia kujiuzulu kutoka baraza la mawaziri la Netanyahu na sasa wametangaza kutoka katika chama chao hicho na kuunda chama kipya cha mrengo wa kulia.
Tovuti ya gazeti la Kizayuni la "Times of Israel" imeandika kuwa Nafati Bennet kinara wa chama cha "Nyumba ya Mayahudi" ambaye ni waziri wa elimu katika baraza la mawaziri la Netanyahu na Ayelet Shaked waziri sheria wa utawala huo ghasibu ambao ni wanachama wakuu wa chama hicho wametangaza kujiondoa katika chama chao na kuunda chama kipya ambacho wamekipa jina la "Mrengo Mpya wa Kulia"(Hayemin Hehadash). Chama hiki kimeundwa kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa Aprili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.
Uchunguzi wa maoni pia umepelekea wapinzani wa Netanyahu kupata matumaini ya kuchukua uongozi. Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na kanali ya 12 ya televisheni ya Isarel siku tano zilizopita yamebaini kuwa asilimia 52 ya Wazayuni hawataki kumuona tena Netanyahu akiwa waziri mkuu.
Nukta ya mwisho ni kuwa, kabla ya kufanyika uchaguzi kutashuhudiwa ushindani mkali zaidi baina ya vyama vya mrengo wa kulia; na matumaini ya Netanyahu, ambaye Avi Gabbay, kiongozi wa chama cha Leba cha utawala wa Kizayuni, amemwita "mwanasiasa fisadi", yataendelea kudidimia.