Sayyid Hassan Nasrullah: Uwezo wa muqawama wa Hizbullah umeongezeka zaidi
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa uwezo wa muqawama ambao unazidi kuongezeka kila siku, ni urithi wa makamanda waliouawa shahidi na alama ya nguvu ya harakati hiyo na kwamba njia hiyo itaendelea daima.
Sayyid Hassan Nasrullah ameyasema hayo katika marasimu ya kuenzi makamanda waliouawa shahidi yaliyopewa jina la Hudaatu al-Darb (waongozaji wa njia), na kusisitiza kwamba Marekani na utawala haramu wa Israel zimefanya kila jambo zinaloweza katika miaka iliyopita lakini zimeshindwakufikia malengo ziliyoyakusudia. Ameongeza kwamba katika suala hilo, ni muqawama pekee ndio unaoainisha mlingano wa kuingia katika duru za ushindi na kwamba siri ya nguvu ya muqawama huo si tu kwamba ni kumiliki silaha, bali ni uwezo mkubwa wa imani na irada thabiti. Amesema kwamba madamu mambo hayo bado yapo, basi muqawama utaendelea kufanya maandalizi ya lazima kwa ajili ya kukabiliana na vita vyovyote tarajiwa vya adui. Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayydi Hassan Nasrullah ameashiria juu ya ushiriki mkubwa wa makumi ya mamilioni ya watu katika sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye nguvu kiasi cha kumfanya adui yeyote asithubutu kuishambulia kijeshi na kwamba ushiriki huo mkubwa wa wananchi umetoa jibu kali kwa vitisho na vikwazo vya maadui wa Iran.
Kadhalika Sayyid Hassan Nasrullah ameongeza kuwa, lengo la mkutano wa hivi karibuni ulioitishwa mjini Warsaw, Poland dhidi ya Iran, lilikuwa ni kuboresha uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni, kuuweka wazi uhusiano huo baada ya kuwa wa siri, kumuunga mkono Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel na kuizingira Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha sambamba na kutangaza uungaji mkono wake kwa serikali halali ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela inayokabiliana na njama chafu za Marekani, amesema kuwa madai yanayotolewa na viongozi wa Marekani juu ya kuwepo kambi za kijeshi za Harakati ya Hizbullah nchini Venezuela ni yenye kuchekesha na kuongeza kwamba, Hizbullah haina ofisi yoyote yenye uhusiano nayo katika eneo zima la Amerika ya Latini. Kadhalika amezungumzia vita vya Yemen na kuvitaja kuwa ni vita vya utawala haramu wa Israel na Marekani ambavyo vinatekelezwa na Saudi Arabia na Imarati.