Golan, sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi ya Syria
Hivi karibuni na kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Donald Trump wa Marekani alidai kuwa utawala haramu wa Israel unayo mamlaka ya utawala wa miinuko ya Golan.
Naye Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo khabithi akayaelezea madai hayo ya Trump kuwa ni "hatua ya kishujaa." Hata hivyo ukweli unabaki kuwa, miinuko ya Golan, ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi ya Syria. Katika vita vya siku sita hapo mwaka 1967, utawala haramu wa Israel na bila kuzingatia sheria, uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan, ambayo ni milki ya Syria. Kwa kipindi cha miaka 52 sasa utawala huo umefanya juhudi nyingi kwa ajili ya kuiunganisha miinuko hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), lakini si Syria pekee, bali jamii yote ya kimataifa haijakubali katu madai ya Tel Aviv ya kudhibiti miinuko hiyo. Katika uwanja huo azimio nambari 242 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni miongoni mwa nyaraka muhimu za jamii ya kimataifa ambazo zilitupilia mbali madai ya Israel ya kutaka kujimilikisha miinuko hiyo ya Golan. Azimio hilo linapinga udhibiti wa maeneo yaliyotwaliwa kupitia vita, kama ambavyo Israel nayo iliikalia kwa mabavu miinuko hiyo kupitia vita vya siku sita. Kuhusiana na suala hilo, Richard Nathan Haass, Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni nchini Marekani, sambamba na kupinga hatua ya Rais Donald Trump ya kujaribu kuutambua rasmi umiliki wa Israel kwa milima hiyo ya Syria, ameitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa usalama wa eneo la Asia Magharibi na amesisitiza kwamba, msingi mkuu wa mfumo wa kimataifa ni kupinga udhibiti wa maeneo yanayotwaliwa kwa vita, suala ambalo pia limekiukwa wazi na Trump.
Inafaa kuashiria kuwa, baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani, uvamizi na ukaliaji mabavu wa Israel umeongezeka zaidi, na hii ni kwa kuwa mbali na Israel kuendeleza jinai nyingi zikiwemo za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, Trump pia amekuwa akitekeleza maamuzi yasiyozingatia hata kidogo sheria, kuuhusu mji wa Quds wa Palestina na hivi sasa dhidi ya milima ya Golan, ambayo ni milki halali ya Syria. Maamuzi hayo ya rais wa Marekani yanahesabiwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel kuwa ni fursa kwa ajili ya kuzidisha mienendo ya kupenda kujitanua na ya uvamizi. Katika uwanja huo, mwezi Oktoba mwaka jana utawala haramu wa Kizayuni uliendesha uchaguzi wa kieneo kwa ajili ya kujimilikisha rasmi milima ya Golan, uchaguzi ambao hata hivyo ulihudhuriwa na idadi ndogo sana ya wakazi wa Golan. Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria iliandika barua mbili kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja huo ikionyesha upinzani wake mkali kwa hatua hiyo ya kichokozi ya Israel na kusisitiza kwamba, milima ya Golan ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Syria; na kwamba kama si sasa, basi ni katika wakati ujao, lakini Syria itatumia nyenzo zilizo kwenye uwezo wake kuhakikisha inaikomboa miinuko hiyo kutoka kwenye makucha ya wavamizi wa Kizayuni.
Ukweli ni kwamba, hatua za kijuba za Trump zinalenga kwenye uchaguzi ujao wa bunge la Israel. Uchaguzi huo wa kabla ya wakati ndani ya Israel utafanyika tarehe 9 Aprili mwaka huu, kwa hivyo hatua hiyo ya rais huyo wa Marekani inalenga kumfagilia njia ya ushindi Netanyahu kwenye uchaguzi huo. Kwa upande mwingine ni kwamba, Trump anafanya njama pia za kuvutia uungaji mkono wa lobi ya Kizayuni kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 nchini Marekani, na hii ni katika hali ambayo kiongozi huyo anakabiliwa na mashinikizo mengi ya ndani. Ama nukta ya kufaa kuhitimishia ni kwamba, uamuzi usiozingatia sheria wa Rais Donald Trump wa Marekani katika kujaribu kuutambua rasmi umiliki wa utawala katili wa Israel kwa miinuko ya Golan ya Syria, umekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka nchi mbalimbali za dunia. Katika uwanja huo, Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki sambamba na kutangaza kwamba nchi yake inaunga mkono umoja wa ardhi yote ya Syria sambamba na kupinga uamuzi huo wa Trump, amesema kuwa, hatua ya rais huyo wa Marekani itashadidisha migogoro katika eneo la Asia Magharibi. Mbali na Uturuki, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nazo pia zimeonyesha upinzani wao mkali dhidi ya njama ya kutaka kuuhalalisha rasmi udhibiti wa Israel kwa miinuko hiyo. Aidha upendeleo na ukereketwa usiozingatia mantiki wa serikali ya Trump kuuhusu utawala khabithi wa Israel, vinaweza kuandaa mazingira ya vita na machafuko zaidi katika eneo la Asia Magharibi, kama ilivyokuwa kwenye hatua ya kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu wa Israel na pia hatua ya Washington ya kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv na kuupeleka mji huo ambayo ilipelekea kuibuka wimbi jipya la Maandamano ya Haki ya Kurejea. Maandamano ambayo hadi sasa yamepelekea karibu Wapalestina elfu 27 kuuawa na kujeruhiwa.