Marekani yaafiki kuiuzia Saudi Arabia teknolojia ya siri ya nyuklia
Taarifa zilizofichuka zimebaini kuwa, Marekani imeuuzia utawala wa Saudi Arabia siri za nyuklia.
Shirika la Habari la Reuters limesema limepata nyaraka za siri ambazo zinaonyeshoa kuwa, Rick Perry, waziri wa nishati wa Saudi Arabia ameidhinisha mashirika ya Marekani yaiuzuie Saudi Arabia teknolojia ya siri ya nyuklia.
Shirika hilo la habari mwezi uliopita pia lilifichua kuwa maafisa wa serikali ya sasa na zilizopita Marekani walihusika katika jitihada za kuiuzia Saudi Arabia siri za nyuklia pamoja na kuwa wanachama wa Baraza la Usalama wa Taifa Marekani walipinga suala hilo.
Herbert McMaster ambaye amewahi kuwa mashauri wa usalama wa taifa wa Marekani ni kati ya watu ambao walipinga vikali Saudia kuuziwa siri za nyuklia.
Maafisa wa usalama na wanasiasa Marekani wana hofu kuwa, Rais Donald Trump anaendeleza mpango wa kuiuzia Saudi siri za nyuklia katika hali ambayo hakuna dhamana Saudia itatumia ipasavyo siri hizo. Wamebainisha wasiwasi wao kuwa yamkini jambo hilo likageuka na kuwa tishio kwa usalama wa taifa wa Marekani.
Wakuu wa Marekani wanaiuzia Saudia teknolojia ya nyuklia katika hali ambayo wanapinga hatua yoyote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif aliitaja hatua hiyo ya Marekani kushirikiana na Saudia katika uga wa nyuklia kuwa ni ya kindumakuwili.