Bunge la Iraq lakosoa vikali harakati za kutia shaka za balozi mdogo wa Marekani nchini humo
(last modified 2019-04-16T04:08:04+00:00 )
Apr 16, 2019 04:08 UTC
  • Bunge la Iraq lakosoa vikali harakati za kutia shaka za balozi mdogo wa Marekani nchini humo

Kamati ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq sambamba na kukosoa vikali harakati za kutia shaka za balozi mdogo wa Marekani mjini Baghdad, imesisitiza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq inatakiwa kuchukua hatua kuhusiana na suala hilo.

Mahdi Taqi, mjumbe wa kamati hiyo ameyasema hayo katika mahojiano na mtandao wa habari wa al-Maalumah na kuongeza kwamba, safari ya Joey Hood, balozi mdogo wa Marekani mjini Baghdad katika eneo la Amiriyah, Fallujah katikati ya Iraq, ilikuwa na lengo la kuwashawishi baadhi ya viongozi wa makabila ya nchi hiyo ili wakubali kuendelea kubakia askari wa Kimarekani ndani ya ardhi ya Iraq. Mahdi Taqi amesisitiza kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq haikuwa na taarifa yoyote kuhusiana na safari hiyo na kwamba suala hilo lilifanyika kinyume na misingi ya udiplomasia kama ambavyo limekiuka haki ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.

Joey Hood, mwambata wa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad anayefanya hila za uchochezi

Aidha kiongozi huyo amesema kuwa hatua ya Hood ni kinyume na ngazi ya uwakilishi wa kidiplomasia na hivyo amekosoa vikali uungaji mkono wa Washington kwa baadhi ya makundi na kuyashawishi kwa ajili ya kufikia malengo yake machafu ndani ya nchi hiyo. Uingiliaji wa kijeshi wa moja kwa moja wa Marekani nchini Iraq na kisha kuikalia kijeshi nchi hiyo, si tu kwamba haujarejesha usalama wa nchi hiyo ya Kiarabu, bali umepelekea kuzalishwa wimbi la makundi ya kigaidi likiwemo genge la kigaidi na ukufurishaji la Al-Qaidah na kisha Daesh (Isis).

Tags