Mwanamke mwenye saratani afia gerezani Imarati licha ya indhari ya UN
(last modified Sun, 05 May 2019 14:19:23 GMT )
May 05, 2019 14:19 UTC
  • Mwanamke mwenye saratani afia gerezani Imarati licha ya indhari ya UN

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeripoti kuwa, mwanamke aliyekuwa anaugua ugonjwa wa saratani amepoteza maisha akiwa gerezani katika Umoja wa Falme za Kiarabu, miezi miwili baada ya Umoja wa Mataifa kutoa mwito wa kuachiwa huru mwanamke huyo kwa misingi ya kwenda kupatiwa matibabu.

Tovuti ya habari ya al-Arab al-Jadid imenukuu watetezi wa haki za binadamu wakisema kuwa, mwanamke huyo kwa jina Alia Abdulnoor amepoteza maisha kutokana na kunyimwa huduma za matibabu, akiwa katika gereza la al-Wathba huko Abu Dhabi, mji mkuu wa Imarati.

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Februari mwaka huu walitahadharisha juu ya kuzidi kuwa mbaya hali ya mwanamke huyo kutokana na kunyimwa matibabu na kuzuiliwa katika mazingira mabaya, ikiwemo kufungwa minyororo akiwa gerezani, kufumbwa macho kwa kitambaa cheusi kwa siku kadhaa, kuzuiwa kukoga na kuzuiwa kuonana na watu wa familia yake.

Familia ya Alia Abdulnoor imeambia Human Rights Watch kwamba, mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 42 alikamatwa nyumbani kwake Imarati Julai 28 mwaka 2015, kwa kuwapa msaada wa kifedha familia kadhaa za wananchi wa Syria mwaka 2011, muda mfupi baada ya kuanza mapigano katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Hata hivyo vyombo vya usalama vya Imarati vilidai kuwa vimemtia mbaroni mwanamke huyo kwa kufadhili harakati za kigaidi. Mwanamke huyo aliyekuwa anauagua kensa ya matiti alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na Mahakama ya UAE mwaka 2017.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika

Familia ya mwanamke huyo imesema Ali Abdulnoor alishurutishwa na maafisa wa serikali ya Imarati kusaini nyaraka zinazoonesha kuwa eti amekataa kufanyiwa matibabu kwa khiari yake.

Februari 26 mwaka huu, Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika alionya kuwa, "Alia anapaswa kuachiwa huru ili akatibiwe na awe karibu na jamaa zake, na wala sio kufungwa pingu kitandani na kuozea gerezani."

Alibainisha kuwa, kesi ya Alia sio ya kwanza wala ya kipekee, na kusisitiza kuwa watawala wa UAE wanapaswa kuacha mchezo wa kuigiza, na badala yake waheshimu mfumo wa sheria na haki za binadamu.