Droni ya Imarati yatunguliwa nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53880-droni_ya_imarati_yatunguliwa_nchini_libya
Jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya limetangaza kuwa, limefanikiwa kutungua ndege moja isiyo na rubani (droni) ya serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 03, 2019 04:18 UTC
  • Droni ya Imarati yatunguliwa nchini Libya

Jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya limetangaza kuwa, limefanikiwa kutungua ndege moja isiyo na rubani (droni) ya serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Mtandao wa al Quds al Arabi umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al Sarraj na ambayo inatambuliwa rasmi na jamii ya kimatafa ukiwemo Umoja wa Mataifa, limefanikiwa kutungua ndege hiyo ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika anga ya Tripoli.

Jana Jumapili mitandao ya kijamii ilienea picha na video zinazoonesha mabaki ya ndege hiyo yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza yakionesha kuwa imetengenezwa nchini Imarati. Ikumbukwe kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa Jenerali Khalifa Haftar ambaye mwezi Aprili mwaka huu alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu huo wa Libya, Tripoli.

Moja ya mabawa ya ndege isiyo na rubani ya Umoja wa Falme za Kiarabu iliyotunguliwa katika anga ya Tripoli, mji mkuu wa Libya

 

Siku chache zilizopita, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, zaidi ya watu 90 elfu wamekuwa wakimbizi huko Tripoli tangu Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji huo.

Tarehe 4 Aprili mwaka huu Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri ya kushambuliwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Jenerali huyo muasi anaungwa mkono na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa. Hata rais wa Marekani, Donald Trump alimpigia simu jenerali huyo akitangaza uungaji mkono wake kwa kile alichodai ni kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa visima vya mafuta vya Libya.