Mauzo ya silaha za Ufaransa kwa Saudia yaongezeka kwa 50%
Ripoti mpya inaonesha kuwa mauzo ya silaha za Ufaransa kwa Saudi Arabia yaliongezeka kwa asilimia 50 mwaka uliopita wa 2018.
Ripoti ya kila mwaka ya serikali ya Ufaransa iliyotolewa leo Jumanne imesema, Paris iliiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni 9 mwaka jana 2018, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 ya mauzo ikilinganishwa na mwaka juzi.
Tony Fortin, afisa wa shirika la kutathmini mauzo ya silaha la Observatory of Armaments lenye makao makuu mjini Paris amezungumzia ripoti hiyo na kusema: "Mauzo hayo ya silaha yanaweka wazi kuwa, mgogoro wa Yemen au Pembe ya Afrika utazaidi kupanuka."
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly amehalalisha mauzo hayo kwa kudai kuwa: "kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi hizo (Saudia na Imarati) kunamaanisha kuimarika uwepo wetu katika maeneo muhimu kwa maslahi ya usalama wetu na sekta yetu ya nishati. Mauzo hayo pia yanalenga kupambana na ugaidi na kuwadhaminia usalama raia wetu katika eneo hilo."
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian na bila ya kuashiria misaada ya silaha ya nchi yake kwa muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen, alisema kuwa Saudia na Imarati zinatakiwa kuhitimisha 'vita vichafu' ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Inafaa kuashiria kuwa Ufaransa ni mshirika mkubwa wa Marekani na Uingereza pamoja na waitifaki wake wengine wa Ulaya katika kuudhaminia silaha haribifu muungano vamizi wa Saudia na Imarati katika kuishambulia kijeshi Yemen, mashambulizi ambayo yamepelekea zaidi ya watu elfu 16 kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu Machi 2015 hadi sasa.