Mahakama ya Saudia yamhukumu kifo mfungwa wa kisiasa wa Qatif
-
Wafungwa wa kisiasa wanakatwa vichwa Saudi Arabia
Mahakama ya utawala wa Saudi Arabia imemhukumu kifo mfungwa wa kisiasa mkazi wa jimbo la Waislamu wa madhehebu ya Shia la al Sharqiyyah katika mji wa Qatif.
Kituo cha habari cha al A'hd cha Lebanon kimeripoti kuwa, mahakama ya Saudi Arabia jana Jumatatu na baada ya kikao cha kimaonyesho katika kesi iliyokosa vigezo vya kimataifa na vya kiadilifu, ilitoa hukumu ya kifo dhidi ya mfungwa wa kisiasa wa eneo la Qatif, Ali al Rabi'.
Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia ndio wanaounda idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa nchini humo. Waislamu hao ndio wengi zaidi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo inayotawaliwa na ukoo wa Aal Saud.
Tarehe 23 Aprili mwaka huu watu 37 waliuawa kwa kukatwa vichwa nchini Saudi Arabia na wengi wao waliuawa kwa tuhuma za kushirikia katika maandamano ya amani dhidi ya utawalawa kifalme wa nchi hiyo.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa vikali ukandamizaji wa uhuru wa kusema, kunyongwa wapinzani na kufungwa jela waandamanaji na watetezi wa haki za binadamu nchini Saudia. Mashirika hayo yanaitaja Saudi Arabia kuwa ndiye mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.