Netanyahu katika njiapanda baada ya kubwagwa kwenye uchaguzi
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu ameingiwa na kiwewe baada ya kubwagwa katika uchaguzi wa Bunge la Israel (Knesset).
Wakuu wa chama kilichopata kura nyingi katika uchaguzi huo cha Blue and White wanamtuhumu Netanyahu kuwa anataka kuutumbukiza utawala huo katika uchaguzi mwingine wa tatu, na anachopaswa kufanya ni kujiuzulu mara moja.
Yair Lapid, afisa wa ngazi za juu wa chama hicho amesema, "mtu mmoja anayeandamwa na mafaili ya ufisadi anataka tushindwe kuunda serikali ya muungano wa kiliberali. Anapaswa kujiuzulu mara moja."
Naye Benny Gantz, mgombea wa chama hicho aliyembwaga Netanyahu katika uchaguzi huo, amesema iwapo Netanyahu anataka serikali ya muungano, sharti yeye (Gantz) awe Waziri Mkuu.
Chama cha White and Blue kimejizoea viti 33 vya Bunge la Israel lenye viti 120, huku chama cha Netanyahu cha Likud kikiambulia viti 31. Hakuna chama kilichopata kura zinazoweza kukifanya kiunde serikali, na kinachosubiriwa sasa ni uundwaji wa serikali ya muungano.
Netanyahu amejikuta katika njiapanda kutokana na matokeo mabaya kwenye uchaguzi huo na kutokana na pigo hilo, amelazimika kufuta mpango wake wa kushiriki mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaotazamiwa kufanyika baadaye mwezi huu mjini New York.