Ansarullah: Saudia na Imarati zinashirikiana na Israel dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61705-ansarullah_saudia_na_imarati_zinashirikiana_na_israel_dhidi_ya_waislamu
Kiongozi wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah amezionya vikali Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya kuendeleza njama za kutaka kuufanya wa kawaida uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba, Riyadh na Abu Dhabi zinashirikiana na Tel Aviv ambayo inajulikana ni adui mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 20, 2020 04:03 UTC
  • Ansarullah: Saudia na Imarati zinashirikiana na Israel dhidi ya Waislamu

Kiongozi wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah amezionya vikali Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya kuendeleza njama za kutaka kuufanya wa kawaida uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kwamba, Riyadh na Abu Dhabi zinashirikiana na Tel Aviv ambayo inajulikana ni adui mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu.

Abdul-Malik Badreddin al-Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema hayo katika hotuba iliyorushwa hewani kwa njia ya televisheni kutoka Sana'a, mji mkuu wa Yemen na kueleza bayana kuwa: Nchi mbili hizo za Ghuba ya Uajemi zinashirikiana na Israel kuhujumu kadhia ya Palestina.

Amebainisha kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa zikiifuata kibubusa Marekani na utawala dhalimu wa Israel, tawala ambazo kimsingi zinataka kuudhibiti umma wa Kiislamu na kupora rasilimali zao.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, muqawama uliojikita barabara katika mafundisho ya Kiislamu ndiyo stratejia bora zaidi ya kukabiliana na maadui wa Uislamu katika eneo la Asia Magharibi.

Marekani na Israel zinatumia "Muamala wa Karne" kuvuruga umoja wa Waislamu

Abdul-Malik Badreddin al-Houthi ameeleza kinagaubaga kuwa, "Marekani na Israel zinataka kuwafanya watumwa wananchi wa Yemen. Njama zao zinaulenga umma mzima wa Kiislamu. Njama hizo zinalenga kuyafarakanisha mataifa ya Kiislamu ndani kwa ndani, kwa kupanda mbegu za chuki na uhasama miongoni mwao."

Amesema Waislamu wanapaswa kuzinduka na kutoa kipaumbele kwa stratejia ya pamoja ya kuzima njama hizo za Marekani na Israel, tawala ambazo zinataka kuvunja umoja wa Waislamu kwa kupanda mbegu za chuki na mifarakano ya kimadhehebu.