Hamas: Kubadilishana mateka, njia pekee ya Israel kuwapata mateka wake
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni itawapata wanajeshi wake waliotekwa nyara kupitia tu mpango wa kubadilishana mateka.
Hazem Qassem ameeleza kuwa, kuwepo mpangp wenye kueleweka na mazungumo ya moja kwa moja ndio njia pekee inayoweza kutatua suala la kubadilisha mateka kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni.
Huko nyuma pia Ben Gantz Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni aliashiria kukamatwa mateka na Hamas wanajeshi wawili wa utawala huo na kueleza kuwa, hatua za maendeleo kuhusu Ukanda wa Ghaza hazitachukuliwa bila ya kurejeshwa mateka.
Utawala wa Kizayuni unadai kuwa wanajeshi hao wawili waliuawa katika vita vya mwaka 2014; na kwamba Hamas ina miili yao pamoja na mateka wake wengine.
Wakati huo huo, muqawama wa Palestina umekataa kutoa maelezo kuhusu wanajeshi hao wawili wa Israel na unafanya jitihada kuhakikisha maelfu ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel wanaachiwa huru kupitia oparesheni ya kubadilishana mateka. Wapalestina 6,500 wanashikiliwa katika jela mbalimbali za utawala wa Kizayuni hadi sasa. Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za karibuni za Taasisi ya Masuala ya Mateka na Wafungwa wa Zamani wa Kipalestina.