Utawala wa Kizayuni waendelea kufanya wizi katika ardhi za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69380-utawala_wa_kizayuni_waendelea_kufanya_wizi_katika_ardhi_za_wapalestina
Chombo kimoja cha Palestina kimelalamikia vikali jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kupora ardhi za Wapalestina hususan katika mji wa Quds Mashariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2021 03:01 UTC
  • Utawala wa Kizayuni waendelea kufanya wizi katika ardhi za Wapalestina

Chombo kimoja cha Palestina kimelalamikia vikali jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kupora ardhi za Wapalestina hususan katika mji wa Quds Mashariki.

Gazeti la al Quds al Arabi limetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa Ofisi ya Taifa la Palestina ya Kulinda Ardhi na Muqawama imesema katika ripoti yake kwamba baadhi ya mashirika ya Israel katika nchi za Magharibi, yanatumia majina bandia ili yasijulikane kuwa ni ya utawala wa Kizayuni na yananunua kwa bei ghali ardhi za pambizoni mwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na baadaye kuwapa Wazayuni.

Ripoti ya ofisi hiyo iliyoko chini ya Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO imesema kuwa, kuna taasisi 23 kubwa na maarufu za walowezi wa Kizayuni katika upande wa Mji Mkongwe wa Quds ambazo zinanunua mali na ardhi za Wapalestina kwa bei ya juu au yanatumia hati bandia kuwapora Wapalestina mali na ardhi zao.

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Huku hayo yakiripotiwa, juzi Alkhamisi, utawala wa Kizayuni ulipasisha mpango wa kuporwa hekta 14.7 zaidi za ardhi za Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, shughuli zote za Israel za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni kinyume cha sheria. Hata hivyo utawala wa Kizayuni unakaidi marufuku hiyo, kila leo unavunja nyumba za Wapalestina, kuwapora ardhi na mashamba yao na kujenga vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni bila ya kuchukuliwa hatua yoyote na Umoja wa Mataifa.