Netanyahu atupwa nje, Waisraeli washangilia, dunia yapongeza
Benjamin Netanyahu ametimuliwa madarakani na kufikia tamati utawala wake wa miaka 12 katika utawala wa Kizayuni wa Israel. Hii ni baada ya bunge la utawala huo haramu (Knesset) kupiga kura ya kuidhinisha serikali mpya ya muungano jana Jumapili.
Kiongozi wa mrengo wa kulia wa chama cha Yamini (New Right), Naftali Bennett tayari ameapishwa kurithi mikoba ya Netanyahu, ambapo ataongoza kile kilichotajwa kuwa serikali ya mageuzi.
Bennett atakuwa Waziri Mkuu hadi mwezi Septemba 2023, na kisha atamkabidhi Yair Lapid, kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yesh Atid, kuongoza kwa miaka mingine miwili.
Waisraeli wamemiminika mabarabarani na mitaani kwa shangwe na vifijo kusherehekea hatua hiyo ya kutimuliwa madarakani Netanyahu, ambaye wamekuwa wakimtaja kama "Waziri wa Jinai."
Viongozi mbali mbali duniani, wakiwemo waitifaki wa utawala huo khabithi kama Rais wa Marekani Joe Biden na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel tayari wametuma salamu za pongezi kwa Bennett, wakisema kwamba wako tayari kufanya kazi naye.

Tangu mwezi Mei mwaka jana 2020, Netanyahu anapambana na kesi kadhaa za ufisadi, utapeli, kufilisi mali n.k, na sasa baada ya kutimuliwa madarakani, hana kinga yoyote ya kutoshitakiwa.
Bennett ambaye ana misimamo ya kuchupa mipaka ya mrengo wa kulia, amekuwa akitangaza wazi wazi misimamo yake hasi dhidi ya kuundwa taifa huru la Palestina; na kama Nentanyahu, ni mpinzani mkubwa pia wa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.