Imarati yawapa uraia maelfu ya Wazayuni ndani ya miezi 3
Raia wapatao 5,000 wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamepewa uraia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Tovuti ya kuvujisha uovu wa watawala wa UAE ya 'Emirates Leaks' imenukuu vyanzo vya habari vikithibitisha habari hiyo na kuripoti kuwa, Imarati imewapa Wazayuni hao uraia kwa kisingizio kuwa ni wawekezaji.
Tovuti hiyo imeripoti kuwa, Wazayuni waliopewa uraia na Imarati kwa madai kuwa ni wajasiriamali na wawekezaji katika nchi hiyo ya Kiarabu hususan katika miji ya Abu Dhabi na Dubai, hawatahitaji viza wala kukana uraia wao wa Israel.
Haya yameripotiwa siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid, kuitembelea UAE na kufungua rasmi ubalozi wa utawala huo wa Kizayuni katika mji mkuu Abu Dhabi, na pia ubalozi mdogo wa utawala huo pandikizi mjini Dubai, licha ya kuwa ubalozi huo ulikuwa umeanza kufanya kazi miezi mitano iliyopita.
Mapema mwezi uliopita, Imarati nayo ilifungua rasmi ubalozi wake mjini Tel Aviv, siku chache tu baada ya dunia kushuhudia jinai na mauaji ya kutisha ya zaidi ya Wapalestina 250 wa Ukanda wa Gaza, yaliyofanywa na jeshi katili la Israel.
Umoja wa Falme za Kiarabu Septemba mwaka jana ilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni nchi ya kwanza ya Kiarabu kufanya hivyo baada ya kipindi cha miaka 26. Baadhi ya tawala za Kiarabu kama Sudan, Bahrain na Morocco zimefuata mkumbo huo kibubusa.