Israel na duru mpya ya mivutano ya kiusalama na Muqawama
Hatua za karibuni za Israel nje ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu zinaonyesha kuwa utawala huo unalielekeza eneo la Magharibi mwa Asia upande wa mivutano na machafuko mapya kwa kutegemea mahesabu yake yasiyo sahihi katika nyanja tatu za kieneo, ndani na kimataifa.
Waziri wa Vita wa Israel Benny Gantz amedai kuwa tawala huo uko tayari kuingia vitani na Iran. Vilevile na baada ya miaka 15 ndege za kivita za Israel zimeyashambulia maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon lengo likiwa ni kuijaribu harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Wakati huo huo nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Israel mara hii zikiongozwa na Uingereza, zimeanzisha vita vya vyombo vya habari dhidi ya Iran na kudai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imehusika katika shambulio dhidi ya meli ya Mercer Street. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni nini malengo ya mivutano hii mpya ya kiusalama ya Israel dhidi ya mhimili wa Muqawama?
Inaonekana kuwa, lengo kuu zaidi la hatua za utawala wa Kizayuni ni kutaka kutoa pigo kwa serikali mpya ya Iran. Hafla ya kukabidhiana madaraka na kuapishwa Rais mpya nchini Iran ilifanyika rasmi juzi Alhamisi, na serikali mpya tayari imeanza kazi. Hii ni katika hali ambayo Rais mpya wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi amesisitiza mara kadhaa suala la kuimarishwa kambi ya muqawama na mapambano dhidi ya uvamizi, sera za mabavu na jinai za Israel dhidi ya waitifaki wa Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kupitia vita vya kisaikolojia kama madai kwamba uko tayari kupigana vita na Iran au kupitia propaganda zake za vyombo vya habari ukishirikiana na Ulaya na Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel umekusudia kukwamisha mipango ya serikali mpya ya Iran ya kusogeza mbele na kufanikisha siasa zake za ndani na kuimarisha muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia. Ukweli ni kuwa Israel na washirka wake wanafanya kila linalowezekana ili serikali mpya ya Iran ianze shughuli zake chini ya mashinikizo.
Lengo jingine muhimu la Israel ni kuvuruga mazungumzo mapya kati ya Iran na kundi la 4+1 kwa ajili ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ambayo yalisita kwa karibu mwezi mmoja uliopita; nchi za Magharibi zikisubiri kuapishwa serikali mpya hapa nchini. Mivutano mipya ya kiusalama dhidi ya Iran na muqawama inatekelezwa katika mwelekeo huo.
Lengo jingine la Israel linahusiana na mchezo wa kuwania madaraka baina ya wanasiasa ambao bado haujamalizika huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Netanyahu ameondoka madarakani baada ya kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 12 na siku 74 huko Israel lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa ndani na nje ya Israel wanaelewa vyema kwamba, serikali ya kupokezana madaraka kati ya Bennet na Lapid si tu kwamba haina mshikamano, bali pia inafanya kazi chini ya kivuli cha woga na wahka wa kumhofia Netanyahu. Duru hii mpya ya mivutano ya serikai ya sasa ya Israel dhidi ya muqawama inafungamana na masuala ya ndani ili kutaka kuonesha kwamba, baraza la serikali ya sasa ya kupokezana madaraka linaweza kulinda usalama vizuri zaidi kuliko serikali ya Netanyahu.
Suala jingine ni kwamba, hadi sasa Israel ingali katika kiwewe na hasira ya matokeo ya vita vya siku 12 vya Panga la Quds hasa baada ya kuvurugika mahesabu yake kuhusiana na nguvu za wanamapambano wa Palestina. Vurugu za sasa pia zinaonesha wazi udhaifu wa Israel; hii ni kwa sababu kwa upande mmoja imeshambulia maeneo yasiyo na wakazi ya kusini mwa Lebanon, na kwa upande mwingine hata hatua hiyo pia haikunyamaziwa kimya, bali imepewa jibu mwafaka na harakati ya Hizbullah ambayo Ijumaa ya jana ilishambulia kwa makumi ya maroketi maeneo yanayokaliwa kwa mabau ya Mashamba ya Shebaa.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Sheikh Naeem Qasim amesema kuhusu mivutao ya sasa huko kusini mwa Lebabon na ardhi zinazokaliwa kwa mavu za Palestina kwamba: “Hizhullah imetangaza waziwazi kwamba itatoa jibu mwafaka kwa shambulizi lolote linalolenga ardhi ya Lebnon.” Amesema: “Hatua iliyochukuliwa na Hizbullah ilikuwa jibu kwa uchokozi wa adui mvamizi ulioshuhudiwa na dunia nzima, na sisi kama Hizbullah, hatuweza kunyamazia kimya uchokozi huo.”
Kwa ujumla ni kwamba, Israel inajua vyema kwamba, haina uwezo wa kuingia katika vita mpya. Kwa msingi wa mahesabu hayo gazti la al Akhbar limeandika kuwa: "Tel Aviv ina woga kuhusiana na wimbi la majibu ya harakati za mapambano; hata hivyo kwa hatua zake hizo, eneo la Magharibi mwa Asia linaelekea kwenye machafuko na mivutano mingine ambayo ni vigumu sana kwa Israel kuweza kukadiria matokeo yake. Vilevile Washington haitaki kuwepo kwa hali kama hiyo.”