HAMAS yasisitiza kusimama kidete muqawama mbele ya uvamizi wa Israel
(last modified Fri, 07 Jan 2022 08:02:13 GMT )
Jan 07, 2022 08:02 UTC
  • HAMAS yasisitiza kusimama kidete muqawama mbele ya uvamizi wa Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, makundi ya muqawama hayataweka mikono yao nyuma na kutazama tu hujuma na jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama huko Palestina iliyotolewa leo imezungumzia hatua za jinai na uvamizi za utawala ghasibu wa Israel na walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, uamuzi wa hivi karibuni wa Israel wa kujenga nyumba mpya katika ardhi unazozikalia kwa mabavu ni uvamizi wa wazi ambao unakinzana wazi na sheria za kimataifa.

Taarifa hiyo imewaonya viongozi wa utawala vamizi wa Israel juu ya matokeo mabaya ya kuendelea hujuma mashambulio na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusisitiza kwamba, makundi ya muqawama hayataweka mikono yao nyuma na kutazama tu hujuma na jinai hizo.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina

 

Ujenzi huo wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni unakwenda sambamba na bomoabomoa ya nyumba za Wapalestina ambapo katika mwaka uliopita pekee wa 2021 jeshi la Israel limebomoa nyumba na taasisi 950 za Wapalestina.

Utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina huku ukipuuza takwa la jamii ya kimataifa la kusimamisha ujenzi huo kwa kukingiwa kifua na Marekani. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.