Wapalestina waishukuru AU kwa kuifukuza Israel kwenye umoja huo wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80070-wapalestina_waishukuru_au_kwa_kuifukuza_israel_kwenye_umoja_huo_wa_afrika
Harakati za muqawama wa Palestina za Hamas na Jihad al Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 07, 2022 01:01 UTC
  • Wapalestina waishukuru AU kwa kuifukuza Israel kwenye umoja huo wa Afrika

Harakati za muqawama wa Palestina za Hamas na Jihad al Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.

Wakuu wa Umoja wa Afrika (AU), jana Jumapili walisimamisha nafasi ya mwanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo na kuunda kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika ikiwemo Algeria kushughulikia suala hilo. Mwezi Julai mwaka jana, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alitangaza kukubaliwa utawala wa Kizayuni kuwa mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Afrika bila ya hata kupigiwa kura suala hilo na wala kushirikishwa wajumbe wengine.

Taarifa kutoka kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU)  ulioanza juzi Jumamosi huko Addis Ababa Ethiopia zilisema jana kuwa umoja huo umesimamisha nafasi ya Israel ya mwanachama mwangalizi ndani ya umoja huo.

Harakati za mapambano ya Kiislamu za HAMAS na Jihad al Islami za Palestina

 

Wapalestina wameipokea kwa fuhara hatua hiyo ya kiungwana ya wakuu wa Umoja wa Afrika. Shirika la habari la FARS limeinukuu harakati ya Jihad al Islami ya Palestina ikisema kuwa, hatua ya kiungwana ya AU ya kusimamisha uanachama wa utawala wa Kizayuni ambao umepasishwa kwa kauli moja na chombo hicho kikubwa zaidi barani Afrika, ni pigo kwa watu wote ambao wameingia kwenye mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Israel. 

Nayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kupitia msemaji wake Hazim Qassim imeushukuru Umoja wa Afrika kwa hatua yake ya kiungwana ya kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo.