Feb 21, 2023 02:26 UTC
  • Tuhuma hizo kwa hizo na zisizo na msingi za Jamhuri ya Azerbaijan dhidi ya Iran

Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan, kwa mara nyingine tena ametoa matamshi dhidi ya Iran bila kuonyesha nyaraka wala ushahidi wowote.

Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan amedai kwa mara nyingine tena kuwa, shambulizi dhidi ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran ni shambulio la kigaidi. Pembeni ya safari yake ya Ujerumani na wakati alipohudhuria Mkutano wa Usalama wa Munich, Ilham Aliyev amerudia madai hayo na kutaka ufanyike uchunguzi wa wazi na kushtakiwa aliyehusika na shambulio hilo. Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Azerbaijan ilikuwa imetangaza kuwa imeishtaki Iran katika jumuiya za kimataifa kuhusiana na tukio lililojiri katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran.

Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan

Madai hayo ya Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan yanarudiwa katika vikao mbalimbali, huku viongozi wa Iran, hususan Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wakiwa wamesisitiza katika mawasiliano na wenzao wa Jamhuri ya Azerbaijan kwamba watalifuatilia suala hilo kwa uzito mkubwa. Wakati huo huo, ukweli ambao umethibitika wazi ni kuwa, shambulio lililofanywa kwenye ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran na mtu aitwaye Yasin Hosseinzadeh halikutokana na malengo ya kisiasa bali lilifanywa kwa sababu za binafsi tu.

Lakini licha ya hayo, viongozi wa Baku walichukua hatua ya haraka ya kuwahamisha maafisa wa ubalozi wao hapa mjini Tehran. Na baada ya uamuzi huo ambao haukuwa sahihi, katika  hatua nyingine ya kushangaza na ya kutafakarisha, viongozi wa Jamhuri ya Azerbaijan walishikilia kwamba hatua aliyochukua Yasin Hosseinzadeh ilikuwa imepangwa na ni ugaidi wa kiserikali, na kwamba eti wanazo nyaraka kuhusiana na suala hilo. Licha ya kutoa dai hilo, hadi sasa viongozi wa Baku na waungaji mkono wao wa nje hawajatoa hati yoyote inayohusiana na suala hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian (kushoto) katika mkutano na waandishi wa habari na balozi wa Jamhuri ya Azerbaijan Ali Alizadeh

Mkabala wa uropokaji wa mara kwa mara unaofanywa na maafisa wa Baku, kutoweka na kutojulikana aliko Bi Golnare Ali Ava, mke wa Yasin Hosseinzadeh, ambaye aliwahi kwenda ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran kwa ajili ya shughuli za kiidara mnamo mwezi Machi 2021, kungali kumegubikwa na siri na utata mkubwa. Inavyoonekana, viongozi wa Baku wameamua kuufunga upesiupesi ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan hapa Tehran ili kukwepa kutoa majibu kuhusiana na utata huo. Kwa kuzingatia ukweli huo na utata mwingi uliopo kuhusiana na hatua binafsi aliyochukua mtu aliyeshambulia u balozi wa Jamhuri ya Azabajan mjini Tehran, inapasa isemwe kuwa: viongozi wa Baku inatakiwa wabebe dhima ya matamshi yasiyo na nadhari wala umakini yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan.

Maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika ngazi ya juu kabisa ya uongozi walilaani kitendo hicho kuanzia siku ya kwanza kilipotokea Januari 27 na kutaka ufanyike uchunguzi wa pamoja na wenzao wa Jamhuri ya Azerbaijan kuhusu tukio hilo. Lakini viongozi wa Baku, ambao walikuwa na wasiwasi wa kuandamwa na masuali ya vyombo vya habari vya Iran ambayo hawana uwezo wa kuyatolea majibu walikimbilia kutoa amri ya kufungwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran. Licha ya ukweli kwamba picha zilizoonyeshwa kutoka kwenye kamera za ubalozi huo zilikuwa zimetiwa mkono na kuungwaungwa kitoto na kwa namna ya kuchekesha, viongozi wa Baku ambao wanadhani jamii ya kimataifa iko pamoja nao, wangali wanaendelea kuipigia upatu kadhia hiyo.

Ukweli ni kuwa rais wa Jamhuri ya Azerbaijan anatoa matamshi bila kuwa na nyaraka wala uthibitisho wowote, jambo linalokwenda kinyume na misingi ya kidiplomasia na kukinzana na sera za urafiki na ujirani mwema. Kutokana na kufuata siasa na sera za kiuadui dhidi ya Iran, baadhi ya duru huru za kisiasa katika eneo zinaamini kuwa sera mpya za serikali ya Ilham Aliyev zinatokana na ushauri anaopewa na maajinabi na madola ya kigeni; na kwa mtazamo wa duru hizo, maadamu ukoo wa Ilham Aliyev ungali unashikilia hatamu za madaraka na mamlaka ya kisiasa ya Jamhuri ya Azerbaijan ni baidi kwamba uhusiano wa nchi hizi mbili jirani na za Kiislamu utaweza kuwa mzuri.

Katika hitimisho la kiujumla inapasa tuseme kuwa: maafisa wa serikali ya Baku na hasa Rais wa Jamhuri ya Azerbaijan, wanajaribu kuhusisha tukio la kawaida na masuala wadhiha na yaliyo wazi kabisa kwa kila mtu duniani. Siku ya Ijumaa, Januari 27, 2023, mwanamume mmoja mwenye silaha alishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan hapa mjini Tehran kwa sababu za binafsi. Mfanyikazi mmoja wa ubalozi aliuawa na wengine wawili walijeruhiwa katika shambulio hilo. Mara tu baada ya tukio hilo, mafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliwasiliana na viongozi wa Jamhuri ya Azerbaijan na kuwahakikishia kwamba tukio hilo si la kigaidi na uchunguzi kamili utafanywa kuhusiana na tukio hilo.

Aliyeshambulia ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan baada ya kutiwa mbaroni

Dakika chache baada ya tukio hilo, kamanda wa polisi wa Tehran alitangaza kuwa, "mshambuliaji, ambaye alifanya kitendo hiki kwa sababu za binafsi, amekamatwa." Lakini serikali ya Baku iliamua kufunga ubalozi wa Jamhuri ya Azabajani mjini Tehran na kuendeleza propaganda dhidi ya Iran katika ngazi ya kimataifa ili kuwafurahisha maajinabi. Pamoja na hayo, propaganda za serikali ya Ilham Aliyev dhidi ya Iran si tu kwamba hazijaweza kufikia lengo lake, lakini pia zimetoa mwanga wa kufichuliwa zaidi sera za Wazayuni.../

Tags