Hizbullah: Mauaji ya makamanda wa muqawama hayatafanikisha njama za Israel
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali mauaji ya kamanda wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na kusisitiza kuwa, mauaji ya makamanda wa muqawama kamwe hayatafanikisha njama za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Taarifa ya Hizbullah imesema jinai ya kihaini dhidi ya Ali Ramzi al-Aswad (31) viungaji mwa Damascus, mji mkuu wa Syria kwa mara nyingine imedhihirisha hulka na dhati ya ukatili ya adui Mzayuni.
Taarifa ya Hizbullah imesisitiza kuwa, mauaji ya makamanda wa muqawama hayatafanikisha njama za utawala wa Kizayuni wa Israel, bali ukatili wa namna hiyo utawafanya watu wawe macho zaidi.
Brigedi ya Quds, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imesema Aswad aliuawa Jumapili viungani mwa Damascus kwa risasi zenye alama za vidole za adui Mzayuni.
Kamanda huyo aliuawa shahidi siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, na Mkuu wa Harakati Jihad Islami ya Palestina, Ziyad Nakhalah kukutana mjini Beirut na kujadili changamoto zinazoukabili mrengo wa mapambano ya Kiislamu (muqawama) huko Palestina, na kusisitiza haja ya kuwepo ushirikiano zaidi wa siku zijazo kati ya harakati hizo mbili kwa njia ambayo itaimarisha zaidi makabiliano na njama za Israel.
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Israel imeongeza mashambulizi katika miji ya Palestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Kutokana na mashambulizi hayo makumi ya Wapalestina wamepoteza maisha na wengine wengi kukamatwa.
Mashambulizi mengi yamelenga Nablus na Jenin, ambapo vikosi vya Israel vimekuwa vikijaribu kuzima muqawama unaoimarika wa Wapalestina katika miji hiyo inayokaliwa kwa mabavu.