Hatua ya kwanza ya Saudi Arabia kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai
(last modified 2023-04-01T13:48:19+00:00 )
Apr 01, 2023 13:48 UTC
  • Hatua ya kwanza ya Saudi Arabia kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai

Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia limeidhinisha uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Jumuiya ya Shanghai ni muungano wa kisiasa na kiusalama unaojumuisha nchi zenye nguvu na muhimu ambayo nchi kama China, Russia, India, Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wanachama wake wa kudumu na rasmi.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni moja ya mashirika ambayo aghlabu ya wanachama wake wana mtazamo na mwelekeo wa Mashariki, na wachambuzi wanaelezea kuwa inaweka mlingano dhidi ya ushawishi wa Magharibi katika eneo hilo. Saudi Arabia imechukua hatua ya kwanza ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Shanghai wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubaliwa rasmi kuwa mwanachama wa shirika hilo mwaka jana. Hatua ya kwanza ya kupata uanachama katika jumuiya hiyo ni kuwa mshirika wa mazungumzo, hatua ya pili ni mwanachama mwangalizi, na hatua ya tatu ni mwanachama rasmi na wa kudumu.

Bin Salman na Xi Jinping

Baraza la Mawaziri la Saudia tayari limeidhinisha kushiriki nchi hiyo katika Jumuiya ya Ushirikiano la Shanghai kama nchi mshirika wa mazungumzo.

Ushiriki wa Saudi Arabia katika Jumuiya ya Shanghai unatambuliwa kuwa ni tukio muhimu. Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi muhimu za Kiarabu zenye uhusiano wa karibu na Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia, na katika miaka miwili iliyopita kumekuwapo hitilafu katika uhusiano wa pande hizo mbili. Mpasuko huo uliifanya Saudi Arabia kuwa karibu na China na kurejesha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vyanzo vya habari vilitangaza kuwa suala la Saudi Arabia kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai lilijadiliwa wakati wa ziara ya Rais wa China, Xi Jinping, mjini Riyadh mwezi Disemba mwaka jana. Katika mwezi uliopita wa Machi China ilifanya upatanishi kati ya Iran na Saudi Arabia na ilikuwa na nafasi kubwa katika kufufua uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Uamuzi wa Baraza la Mawaziri la Riyadh kujiunga na Jumuiya ya Shanghai ulichukuliwa siku moja baada ya Rais wa China, Xi Jinping, kujadili masuala mbalimbali katika mazungumzo yake ya simu na Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman. Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kampuni ya Aramco ya Saudia kutangaza uwekezaji wa mabilioni ya dola nchini China. Kwa msingi huo, uamuzi wa Saudi Arabia wa kuwa mwanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unatathminiwa katika fremu ya kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na China, na unaonyesha kuwa mwelekeo wa Mashariki katika siasa za nje za Saudia unazidi kuimarika.

Suala jingine muhimu ni kwamba Saudia ilifanya uamuzi huo huku Marekani ikiwa na wasiwasi kuhusu ukaribu wa Riyadh na Beijing. Kabla ya hapo pia Washington ilikuwa na wasiwasi kuhusu upatanishi wa Beijing kati ya Tehran na Riyadh na ilijaribu kadiri iwezavyo kuficha wasiwasi huo. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, Riyadh inataka kuanzisha uhusiano imara na wa muda mrefu na China licha ya wasiwasi wa Marekani.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, mienendo na vitendo vya Saudi Arabia vinaonesha kuwa, kujikurubisha kwa China na hata kwa Russia kunatokana zaidi na mabadiliko ya kimtazamo baina ya watawala wa Saudia kuliko kuonyesha kutoridhika na Marekani.

Bin Salman na Biden

Katika miaka ya hivi karibuni, Saudi Arabia imekuwa ikidunishwa na kudhalilishwa mara kwa mara na viongozii wa serikali ya Marekani, na sasa inajaribu kuonyesha uhuru wake katika sera za nje kwa kuimarisha uhusiano na nchi kama China na kwa kueleza nia yake ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Tags