Al Mashat ataka kususiwa bidhaa za Marekani na Wazayuni
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amezitolea wito nchi za Kiarabu na Kiislamu kususia bidhaa za Marekani na za utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina, muqawama na mapambano yao.
Mahdi al-Mashat ametoa taarifa akizitolea wito nchi za Kiarabu na Kiislamu kuwaunga mkono na kuwasaidia wananchi wanaodhulumika wa Palestina. Al Mashat amepongeza jibu halali lililotolewa na makundi yote ya mapambano ya Palestina kwa jinai za kinyama za adui Mzayuni dhidi ya makamanda wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kufuatia mashambulizi ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya makazi ya raia huko Ghaza.
Wakati huo huo Mahdi al-Mashat ametangaza kuwa wananchi na serikali ya Yemen wanaunga mkono machaguo yote yatakayoamuliwa na uongozi wa muqawama wa Palestina ili kujibu hujuma ya kigaidi ya adui Mzayuni.
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen pia ametilia mkazo udharuura wa kushikamana wananchi na harakati za mapambano za Palestina ili kutoa jibu kwa adui Mzayuni na kulitaja jambo hilo kuwa ni hatua muhimu kuelekea ushindi wa Quds na kurejesha haki zote za wananchi madhulumu wa Palestina.
Ndege za kivita za Israel zilianza kushambulia maeneo ya makazi ya raia katika Ukanda wa Ghaza asubuhi ya Jumanne wiki hii; ambapo hadi kufikia sasa Wapalestina 25 wakiwemo watoto, wanawake na makamanda wanne wa ngazi ya juu wa Brigedi ya Quds (Suraya al Quds), tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad Islami ya Palestina wameuawa shahidi.