Mifumo ya ulinzi wa anga ya Hizbullah yaitia wahaka Israel
Gazeti moja la Kiebrania limeripoti kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel linatiwa wasi wasi na mifumo ya ulinzi wa anga ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Kwa mujibu wa gazeti la Maariv, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeingiwa na hofu kubwa baada ya harakati ya muqawama ya Hizbullah kuimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga.
Kwa mujibu wa gazeti hilo linalochapisha habari zake kwa lugha ya Kiebrania, Harakati ya Hizbullah imeongeza maradufu kiwango cha mifumo ya ulinzi inayomiliki katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Aidha gazeti la Maariv limedai kuwa, mifumo ya Hizbullah imeimarishwa na kuundwa kwa kutegemea ujuzi na muundo wa mifumo ya kisasa kabisa ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Hizbullah imekuwa ikiimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga tokea mwaka 2019, baada ya kujiri shambulizi la ndege isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Beirut mwaka huo.
Wakati huo, Hizbullah iliilenga droni ya Wazyuni aina ya Hermes 450 kwa kombora la SA-8 la ardhini hadi angani, kujibu chokochoko za utawala haramau wa Israel kusini mwa mji wa Lebanon.
Baada ya tukio hilo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imejaribu mara tatu kutungua droni za Wazayuni zilizoruka katika anga yake kinyume cha sheria.