Jumuiya ya OANA yataka kulindwa waandishi wa habari Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i103694-jumuiya_ya_oana_yataka_kulindwa_waandishi_wa_habari_gaza
Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia-Pasifiki (OANA) imesisitizia haja ya kudhaminiwa usalama na ulinzi waandishi wa habari walioko katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 19, 2023 23:28 UTC
  • Jumuiya ya OANA yataka kulindwa waandishi wa habari Gaza

Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia-Pasifiki (OANA) imesisitizia haja ya kudhaminiwa usalama na ulinzi waandishi wa habari walioko katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya jana Alkhamisi ya OANA imeeleza kuwa, jumuiya hiyo inatiwa wasi wasi juu ya usalama wa wanahabari wanaofanya kazi katika eneo la mgogoro la Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia-Pasifiki imebainisha kuwa, majukumu ya vyombo vya habari ni kulinda uhuru na utambulisho wa mataifa, na hasa mataifa ya eneo hili.

OANA imesema wanachama wake wamekuwa walengwa wa ukatili huko Gaza, kosa lao tu likiwa ni kufanya kazi yao ya kuakisi uhalisia wa mambo katika ukanda huo ulio chini ya mzingiro.

Nchi wanachama wa OANA zinaunda asilimia 56 ya uzalishaji jumla wa dunia, karibu asilimia 50 ya biashara ya dunia, zaidi ya asilimia 60 ya eneo la maji na zaidi ya asilimia 25 ya usafiri wa anga.

Taarifa ya Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia-Pasifiki OANA imebainisha kuwa, hakuna kitu chochote kinaweza kuhalalisha waandishi wa habari kuwa walengwa wa ukatili unaoendelea Gaza. Imesema hakuna chembe ya shaka kwamba jinai zinazoendelea kufanywa Gaza zinakanyaga haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Baada ya kuanza oparesheni ya "Kimbunga cha Al Aqsa" Oktoba 7, serikali na vyombo vya habari vya Magharibi kwa upande mmoja vilianzisha propaganda kubwa ili kuzuia kuakisiwa habari na matukio yanayojiri huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, huku vikichapisha na kutoa habari za uwongo ili kuonyesha taswira isiyo ya kibinadamu kuhusu wanamapambano wa Palestina.