Dec 03, 2023 10:59 UTC
  • Kombe la Dunia U17; Ujerumani bingwa

Kwa mara ya kwanza, Ujerumani imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa vijana wa kiume wenye chini ya umri wa miaka 17.

Hii ni baada ya kuisasambua Ufaransa katika kitimutimu cha fainali iliyopigwa Jumamosi nchini Indonesia. Vijana hao wa Ulaya walipambana kufa kupona na kutoshana nguvu kwa kuzabana mabao 2-2 katika dakika za ada. Mabao ya Ujerumani yalifungwa na Paris Brunner na Noah Davich, huku ya vijana wa Kifaransa yakifungwa na Saimon Nadelia na Mathis Amougou.

Walilazimika kuingia kwenye upigaji matuta, na hapa ndipo mbivu na mbichi ikabanika, kwa mabarobaro wa Kijerumani kuibuka na ushindi wa magoli 4-3.

Wameibuka kidedea licha ya kujikuta wakicheza wachezaji 10 uwanjani katika dakika 21 za mwisho, baada ya mchezaji wake, Winners Osawe kulishwa kadi ya pili ya njano. Penati iliyotiwa wavuni na Paris Brunner katika kipindi cha kwanza iliwaweka kifua mbele Wajerumani wakicheza fainali kwka mara ya kwanza tokea mwaka 1985. Walizidi kukoleza ushindi wao kwa bao la nahodha Noah Darvich dakika sita baadaye.

Hata hivyo Wafaransa walijikusanya na kusawazisha, na timu mbili hizo zikalazimika kungia kwenye upigaji matumat ili kumpata mshindi wa Kombe la Dunia kwa vijana wasiozidi miaka 17.

Mali ambayo ilimaliza ya pili katika Kombe la Dunia la mwaka 2015, iliichabanga miamba ya soka Argentina mabao 3-0 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na kutunukiwa medali ya shaba katika duru ya mashindano hayo ya Shirikisho la Soka Dunia FIFA mwaka huu. Mabao ya vijana hao wa Afrika Magharibi kwenye mchezo huo wa Ijumaa yalifungwa na Ibrahim Diarra, Mamadou Doumbia na  Hamidou Makalou.

 

Tags