Dec 12, 2023 02:39 UTC
  • Uhalalishaji Marekani kura yake ya turufu kuhusu mauaji ya kimbari ya Wazayuni huko Gaza

Licha ya matakwa ya kimataifa ya kusitishwa mara moja vita vya mauaji ya kimbari ya Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza, lakini Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa utawala wa Kizayuni, imepinga maombi hayo na inaendelea kuwasha moto wa vita hivyo vya umwagaji damu kwa kutuma silaha za kila aina huko Gaza.

Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, katika mahojiano na vyombo vya habari, ameashiria  mojawapo ya sababu za kupinga nchi yake usitishaji vita katika ukanda huo. Katika mazungumzo na  ABC News, Blinken ameeleza hivi sababu ya Marekani kupinga usitishaji vita: "Tunapozungumzia usitishaji vita wakati huu, ambapo Hamas bado imesimama imara, inaendeleza mapambano, haijapata madhara na imeweka wazi  nia yake ya kurudia tena mashambulizi kama yale ya Oktoba 7, suala hilo litaendeleza tu matatizo yaliyopo katika eneo hilo.  Hivi karibuni Marekani ilipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa vita vya Gaza.

Kutokuwa na msingi sababu zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani za upinzani wa Washington dhidi ya usitishaji vita wa Gaza zimeweka wazi ukweli wa mambo kuhusu masuala kadhaa. Blinken amesema kuwa sababu kuu ya upinzani wa Marekani dhidi ya usitishaji vita ni kuendeleza Hamas mapambano. Ni lazima  tujiulize kuwa je, ikiwa baada ya zaidi ya miezi miwili ya vita na mauaji ya maelfu ya watu wa Gaza, utawala wa Kizayuni bado haujaweza kuishinda Hamas au kuiangamiza, suala ambalo pia amelikiri Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, basi ni vipi itafikia malengo yake kwa kuendeleza mashambulizi ya kiholela ya hivi sasa na ya kinyama ambayo yamesababisha maafa na uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza, ambapo makumi ya maelfu ya wakazi madhulumu wa eneo hilo wameuawa kinyama na bila huruma kwa mabomu ya Marekani? Je, kwa kulipua na kushambulia mara kwa mara shule, hospitali, misikiti na hata makanisa, kutawatoa nje wapiganaji wa Hamas na makundi mengine ya muqawama ya Palestina, ambao kwa mujibu wa Tel Aviv, wamejikita  katika mahandaki na mifereji ya mamia ya kilomita katika Ukanda wa Gaza na wamesababisha hasara kubwa kwa wanajeshi na zana  za utawala wa Kizayuni? Kwa hakika utawala wa Biden unaidhinisha hatua za kikatili za utawala wa Kizayuni dhidi ya makundi ya muqawama wa Palestina huko Gaza, licha ya kufahamu vyema kuwa haziwezi kuwa na matokeo yoyote ya maana kwa utawala huo bali zinasababisha maafa na uharibifu mkubwa kwa watu wa Gaza, na hiyo ni kwa sababu tu ya uungaji mkono wake usio na mpaka kwa Israel. Rais Joe Biden wa Marekani daima amekuwa akiutetea utawala huo wa Kizayuni kwa madai kuwa una haki ya kujilinda.

Mashambulizi ya kinyama ya Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza

Hivi karibuni, Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni alisema katika mahojiano kwamba: 'Tunatabiri kuwa vita vya Gaza vitaendelea na kasi yake ya sasa kwa angalau miezi mingine miwili. Baada ya hapo, itafuata operesheni ya "kusafisha"  ili kuangamiza  makundi ya Hamas.' Matamshi hayo yanaonesha kuwa licha ya mashinikizo ya kimataifa ya kutaka kusitishwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, lakini viongozi watenda jinai wa utawala huo bado wanatilia mkazo kuendeleza mashambulizi yao ya kinyama dhidi ya raia wasio na hatia wa Gaza kutokana na uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kwa utawala huo wa Kizayuni. Hii ni katika hali ambayo, hata maeneo yaliyotangazwa kuwa eti ni salama huko Gaza pia yanakabiliwa na milipuko ya mabomu ya askari vamizi wa Israel.  Hadi sasa Wapalestina wapatao 18,000 wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi 2 iliyopita wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake.

Nukta muhimu ni nafasi muhimu ya misaada ya kijeshi ya Marekani katika kuendeleza operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni huko Gaza. Kwa mujibu wa gazeti la Marekani la Washington Post, ripoti zilizowasilishwa katika Bunge la Marekani zinaonyesha kuwa zaidi ya mabomu erevu elfu 22 ya Marekani yamerushwa huko Gaza. Vilevile, katika kipindi hiki, serikali ya Marekani imeukabidhi utawala wa Kizayuni mabomu yasiyopungua 15,000 yakiwemo ya pauni 2,000 ya kupenya kwenye mahandaki na zaidi ya mizinga 50,000 ya milimita 155. Nukta ya kushangaza ni kwamba, mwaka jana, serikali ya Marekani iliunga mkono ombi la kimataifa kuhusu udhibiti wa matumizi ya silaha za milipuko hatari katika maeneo ya mijini.

Maafa ya watoto madhulumu wa Palestina

Licha ya himaya kubwa ya serikali ya Biden , ambayo anadai kuunga mkono haki za binadamu,  kwa Israel, lakini  ndani ya Marekani kwenyewe, na hasa kati ya wananchi na wasomi, upinzani dhidi ya vitendo vya jinai vya Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza na kutaka kusimamishwa haraka vita na kukomeshwa umwagaji damu unaongezeka. Matokeo ya kura ya maoni ya pamoja ya CBS News na taasisi ya Yugao, yaliyotangazwa Jumapili, yanaonyesha kuwa asilimia 61 ya Wamarekani hawakubaliani na sera za Rais Joe Biden wa Marekani kuhusu vita vya Gaza. Utafiti mwingine uliofanyika mwezi Oktoba ulionyesha kuwa asilimia 56 ya Wamarekani hawakukubaliani kabisa na siasa za Biden. Katika ngazi za wasomi na taasisi za kisiasa, pia kuna ongezeko la matakwa ya kubadilishwa sera za utawala wa Biden kuhusu vita vya Gaza. Aidha katika barua ya wanadiplomasia wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na hata wahudumu wa Ikulu ya White House, wametaka kubadilishwa misimamo ya Washington kuhusu vita vya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kuanzishwa usitishaji vita katika eneo hilo haraka iwezekanavyo. Suala muhimu ni kushindwa madai ya Israel na vita vyake vya kipropaganda vya kuhalalisha vitendo vyake vya jinai huko Gaza kufikia malengo yaliyokusudiwa. Suala ambalo hata wanasiasa wa Marekani wanalikiri wazi. Seneta Bernie Sanders wa Marekani amesema Israel haiwezi kuingia vitani dhidi ya wananachi wa Palestina na kusababisha uharibifu wa kutisha  tunaoshuhudia dhidi ya Wapalestina na kuongeza: 'Israel imeshindwa vita katika fikra za  walimwengi kuhusiana na suala hilo.'

 

Tags