CIA: Kundi la Daesh linatumia silaha za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i1081-cia_kundi_la_daesh_linatumia_silaha_za_kemikali
Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limesema kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2016 04:40 UTC
  • CIA: Kundi la Daesh linatumia silaha za kemikali

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limesema kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake.

John Brennan, Mkurugenzi wa CIA amenukuliwa na shirika la habari la CBS News akisema kuwa, wana ushahidi wa kuonyesha kuwa Daesh wanatumia silaha hizo hatari dhidi ya binadamu.

Brennan amefichua kuwa kundi hilo la kigaidi lina ujuzi wa kutengeneza silaha za kemikali kwa kutumia gesi ya klorini na haradali (mustard), kama iliyotumika katika vita vya kwanza vya dunia. Kadhalika Mkurugenzi wa CIA ametahadharisha kuwa, kuna uwezekano wa Daesh kuwauzia Wamagharibi silaha hizo za kemikali ili kupata fedha za kuendeshea harakati zao za kigaidi. Kauli hii inakuja siku mbili baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Kiintelijensia ya Marekani, James Clapper kuiambia Kamati ya Bunge la Kongresi ya nchi hiyo kuwa Daesh wanatumia silaha za kemikali nchini Iraq na Syria.

Hii ni katika hali ambayo, kundi hilo la kitakfiri limekuwa likipata uungaji mkono kutoka Marekani ikishirikiana na waitifaki wake wa eneo hili zikiwemo Saudi Arabia, Qatar na Uturuki, tangu lianzishe hujuma zake dhidi ya Syria Machi mwaka 2011.