Feb 18, 2024 11:05 UTC
  • US kuipigia veto rasimu ya azimio la Algeria la kusitisha vita Gaza

Maafisa wa Marekani wameapa kuwa nchi hiyo itatumia kura yake ya turufu kupinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Algeria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield amesema katika taarifa kuwa, muswada huo hautapasishwa iwapo utawasilishwa kwa ajili ya kupigiwa kura katika Baraza la Usalama.

Duru za kidiplomasia zimesema muswada huo unatazamiwa kupigwa kura Jumanne ijayo. Rasimu hiyo iliyowasilishwa na Algeria katika Baraza la Usalama zaidi ya wiki bili zilizopita, inahitaji kura zisizopungua 9 za wanachama 15 wa baraza hilo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai kuwa, 'Marekani haiunga mkono rasimu hiyo. Iwapo itawasilishwa kwa ajili ya kupigiwa kura kama ilivyo, haitapita. Matini (ya rasimu hiyo) inaweka hatarini mazungumzo hasasi ya usitishaji vita."

Matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani yamekuja huku Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akisisitiza hiyo jana kuwa makubaliano mapya (ya kusitisha vita) 'hayaonekani kuwa karibu.'

Katika hatua nyingine, maelfu ya Wamorocco jana Jumamosi walijitokeza tena kwenye barabara za mji mkuu wao Rabat kutoa wito wa kusitishwa uhusiano wa nchi yao na utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao wameulaani na kuutaja kuwa ni mfanya "mauaji ya kimbari" katika Ukanda wa Gaza.

Wamorocco katika maandamano ya kuwatetea Wapaletina

Maandamano hayo yaliyoandaliwa na makundi mbali mbali yenye mielekeo ya kisiasa ya mrengo wa kulia na mrengo wa kushoto yameshuhudiwa pia katika miji ya Tangier na Casablanca, ambapo waandamanaji sambamba na kuzichoma moto bendera za utawala haramu wa Kizayuni, wametangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina na kutaka kusitishwa vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Aidha muungano wa waungaji mkono wa Palestina jana Jumamosi ulifanya maandamano makubwa katika miji takriban 100 kwenye zaidi ya nchi 45 duniani, ikiwemo miji ya London, Paris, Rome, Berlin, Dublin, Washington, Sydney, Islamabad na Seoul ili kutangaza mshikamano wao na watu wa Gaza.

Tags