Rashida Tlaib amkabili Netanyahu katika Bunge la Marekani kwa kumwita "mhalifu wa kivita"
(last modified 2024-07-25T10:55:26+00:00 )
Jul 25, 2024 10:55 UTC
  • Rashida Tlaib
    Rashida Tlaib

Mwakilishi wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani, Rashida Tlaib amepinga hotuba iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Congress jana, Jumatano, na kutaka awajibishwe kwa mauaji ya kimbari yanayofanyika Ukanda wa Gaza.

Tlaib ambaye alivalia keffiyeh na bendera ya Palestina, wakati wa hotuba ya Netanyahu, aliinua juu bango jeusi lenye maneno "mhalifu wa kivita" katika upande mmoja, na "mtenda jinai ya mauaji ya kimbari" katika upande mwingine.

Rashida Tlaib alisema, "Wapalestina wanastahili kuishi na kukua, na hatutamruhusu waziri mkuu wa Israel mwenye kichaa cha kufanya mauaji ya kimbari kufuta uwepo wetu."

Ameongeza kuwa: Maelfu ya Wapalestina wameuawa katika mauaji haya ya kimbari, na kwamba amehudhuria kikao hicho cha Kongresi na Seneti ya Marekani kilichohutubiwa na Netanyahu ili kukumbusha kwamba, Wapalestina hawatakaa bila kuonekana au kuwa kimya wakati mhalifu wa vita anayetuhumiwa kwa mauaji ya kimbari akihutubia Bunge la Marekani.

Wakati huo huo Tlaib amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Netanyahu ni mhalifu wa kivita anayefanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina, na ni aibu kubwa kuona viongozi kutoka pande zote mbili (Republican na Democratic) wanamwalika kutoa hotuba mbele ya Congress; Netanyahu anapaswa kukamatwa na  kukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko The Hague.”

Maelfu ya watoto wa Palestina wameuawa huko Gaza

Zaidi ya wawakilishi 80 wa Bunge la Congress ya Marekani wamesusia hotuba ya waziri mkuu katili wa Israel, Benjamin Netanyahu. 

Mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina yameua karibu raia elfu 40 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo. Zaidi ya Wapalestina wengine elfu kumi hawajulikani waliko. 

Tags