Mwanamke wa Kimarekani aliyejaribu kumzamisha mtoto wa Kipalestina afunguliwa mashtaka ya jaribio la kuua
(last modified 2024-09-05T02:31:03+00:00 )
Sep 05, 2024 02:31 UTC
  • Mwanamke wa Kimarekani aliyejaribu kumzamisha mtoto wa Kipalestina afunguliwa mashtaka ya jaribio la kuua

Baraza Kuu la Mahakama ya Tarrant limemfungulia mashtaka mwanamke wa Texas kwa tuhuma za kujaribu kumzamisha msichana mwenye umri wa miaka 3 wa Kipalestina raia wa Marekani, kutokana na chuki za ubaguzi.

Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Tarrant imemfungulia mashtaka mshukiwa, Elizabeth Wolfe, 42, katika hati ya mashtaka iliyowasilishwa mwezi uliopita ambayo ni pamoja na kutolewa kwa adhabu kali kwa kufanya uhalifu wa chuki, kulingana na rekodi za mahakama zilizofichuliwa Jumanne wiki hii. Suala hili linaweza kusababisha adhabu kali zaidi kwa Wolf iwapo atapatikana na hatia.

Wolfe anashtakiwa kwa jaribio la kuua, ambalo adhabu yake inaweza kuwa hukumu ya kifo, dhidi ya mtoto wa chini ya umri wa miaka 10, na kusababisha majeraha ya mwili kwa mtoto huyo kwa makusudi.

Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa, tukio hilo lilitokea mwezi Mei mwaka huu katika bwawa la kuogelea katika makazi ya watu eneo la Dallas-Fort Worth, wakati mshukiwa alipozozana na mama wa mtoto huyo, baada ya mtuhumiwa kumuuliza yule mama kuhusu asili yake.

Ripoti ya polisi imeeleza kuwa, mwanamke huyo wa Kimarekani alijaribu kumzamisha mtoto huyo wa Kipalestina na kumshika mtoto mwingine wa mama huyo.

Polisi wamesema kuwa, mama wa mtoto huyo mwenye asili ya Palestina aliweza kumuokoa bintiye kutoka kwenye maji, na kwamba wahudumu wa afya walikimbilia eneo la tukio.

Watetezi wa haki za binadamu wameonya kuhusu ongezeko la vitisho vinavyowakabili Waislamu na Waarabu wa Marekani tangu Israel ilipoanza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Mwezi Oktoba mwaka jana mzungu mwenye umri wa miaka 71 katika jimbo la Illinois nchini Marekani, aliyechochewa na chuki dhidi ya Waislamu na Wapalestina, alimuua kwa kumdunga kisu mara 26 mtoto wa Kiislamu aliyekuwa na umri wa miaka 6 na kumjeruhi vibaya mama yake.

Wadea Al-Fayoume, aliuawa kwa kudungwa kisu huko Marekani

Polisi wa Marekani walisema Joseph Czuba, (71) wa Illinois alimdunga kisu moyoni na kwenye shingo mtoto huyo wa Kiislamu, Wadea Al-Fayoume, huku akimjeruhi vibaya mama yake.

Ripoti zinasema Czuba alikuwa akitoa nara na kauli za kupiga vita Uislamu na Wapalestina wakati anatekeleza ukatili huo. "Mnapaswa kufa, nyinyi Waislamu", amesema Mmarekani huyo huku akimdunga kisu mtoto huyo wa Kipalestina 

Tags