Papa awataka Wakatoliki Marekani wachague 'uovu ulio afadhali kidogo' kati ya Trump na Harris
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewahimiza Wakatoliki nchini Marekani wakapige kura katika uchaguzi wa Novemba, akisema wanapaswa "kuchagua uovu ulio afadhali kidogo" huku akiwakosoa wagombea wote wawili wakuu wa kinyang'anyiro cha urais wa nchi hiyo.
Hata hivyo alikosoa vikali misimamo ya wote wawili akisema, kukataa kuwakaribisha wahamiaji ni dhambi "kubwa" na kutoa mimba ni sawa na "mauaji".
Papa Francis ameendelea kueleza kwamba, kutopiga kura ni kubaya na si vizuri na kwamba ni lazima Wakatoliki wakapige kura; lakini akashauri kwa kusema: "lazima muchague uovu ulio afadhali zaidi," na akahoji: "ni nani mbaya zaidi? Yule bibi au yule bwana? mimi sijui. Kila mtu, ndani ya nafsi yake, [lazima] afikiri na kufanya hivyo (kwa kuchagua uovu ulio afadhali).”
Kiongozi wa Kanisa Katoliki amesema: "iwe ni yule anayefukuza wahamiaji au yule anayeua watoto, wote wawili wanapinga uhai."
Marekani ina Wakatoliki wapatao milioni 52, ambao kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew, takribani asilimia 52 kati yao wanaunga mkono Chama cha Republican, ikilinganishwa na karibu asilimia 44 wanaounga mkono Chama cha Democrat.../