Trump atamka rasmi: Marekani itawahamisha Wapalestina na 'itaitwaa' na 'kuimiliki' Ghaza
(last modified Wed, 05 Feb 2025 05:52:17 GMT )
Feb 05, 2025 05:52 UTC
  • Trump atamka rasmi: Marekani itawahamisha Wapalestina na 'itaitwaa' na 'kuimiliki' Ghaza

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza hadharani kwamba Marekani itachukua udhibiti wa Ukanda wa Ghaza, na kulijenga upya eneo hilo lililoharibiwa na vita na kuandaa fursa za kiuchumi kwa wakazi wake wa baadaye; na alipoulizwa kama atapeleka huko wanajeshi wa Marekani, Trump ameapa "kufanya kitakacholazimu."

Trump ametoa matamshi hayo mbele ya waandishi wa habari kufuatia mkutano wake na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House.

Rais wa Marekani amerudia kauli yake kwamba inapasa Wapalestina wapewe makazi ya kudumu mahali pengine, na akaongeza kuwa Marekani "itaitwaa" Ghaza na kuongoza juhudi za kuondoa uharibifu ulioachwa na miezi 15 ya vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya eneo hilo.

Alipotakiwa na waandishi wa habari afafanue anamaanisha nini hasa kwa anaposema "kuchukua mamlaka," kiongozi huyo wa Marekani alisema, ni kuwa na "umiliki wa muda mrefu" ambao amedai eti utaleta "utulivu mkubwa" katika Mashariki ya Kati nzima.

Trump ameendelea kueleza: "kila mtu ambaye nimezungumza naye analipenda wazo la Marekani la kukimiliki kipande kile cha ardhi, kukiendeleza, na kubuni maelfu ya ajira".

Katika mkutano huo na waandishi wa habari akiwa pamoja na Netanyahu, rais huyo wa Marekani hakufuta uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa nchi hiyo huko Ghaza kwa ajili ya kufanikisha mpango wake aliouita kuwa ni wa maendeleo ya Ghaza.

"Tutafanya kile kitakacholazimu. Ikiwa ni lazima, tutafanya hivyo. Tunakwenda kuchukua mamlaka ya mahali pale", ametamka bila ya aibu kiongozi huyo.

Na alipoulizwa ni nani watakaokwenda kukaa kwenye Ukanda wa Ghaza mara tu baada ya Marekani "kuitwaa" na kuijenga upya, na kama Wapalestina wenyewe wataweza kurejea, Trump alijibu kuwa dunia nzima na wawakilishi kutoka duniani kote watakwenda kuishi huko na kuongeza kuwa ataligeuza eneo hilo kuwa Ukanda wa Pwani wa Mashariki ya Kati wa burudani wa wakati wa mapumziko.../