"US inawakandamiza wafungwa wa Guantanamo, iombe radhi"
(last modified Tue, 27 Jun 2023 06:55:38 GMT )
Jun 27, 2023 06:55 UTC

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amelaani namna Marekani inayoamiliana kikatili na wafungwa walioko katika Gereza la Guantanamo akisisitiza kuwa, Washington inapaswa kuomba radhi kwa jinai na miamala ya kinyama inayofanyiwa wafungwa hao.

Fionnuala Ni Aolain alisema hayo jana Jumatatu katika ripoti yake aliyoitoa baada ya kulitembele gereza hilo la kutisha la Marekani lililoko katika ardhi ya Cuba.

Amebainisha kuwa, "Baada ya kuzuiliwa kwa miongo miwili, madhila na mateso ya wafungwa hao (wa Guantanamo) yanatisha. Ukandamizaji wanaofanyiwa unakanyaga uhuru na haki zao za msingi."

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, pamoja na kuwaweka kizuizini watu kwa kipindi kirefu pasi na kuwasomea mashtaka, vyombo vya dola vya Marekani vinawatesa na kuwaadhibu washukiwa kwa anuai za mateso na adhabu ikiwemo kuwazuia kupumua kwa kuwamiminia maji. 

Wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakiitaka Marekani itekeleze ahadi yake ya kuifunga jela hiyo ya kutisha. Wanasisitiza kuwa, miaka 20 ya uwepo wa jela hiyo inaashiria ukurasa wenye kuchukiza na kutisha wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wa Marekani.

Mateso kwa washukiwa wa ugaidi katika jela ya Guantanamo Bay

Aidha hivi karibuni, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa wito kwa Rais Joe Biden likimtaka atekeleze ahadi yake ya kufunga jela ya Guantanamo. 

Mwaka jana, Cuba ililaani kuendelea kuwepo Jeshi la Marekani katika Hori ya Guantanamo iliyo mashariki mwa nchi hiyo ya Amerika ya Latini, zaidi ya miaka 21 tokea gereza hilo la kugofya la Marekani lifunguliwe katika eneo hilo.

Tangu jela ya Guantanamo ilipoanzishwa Januari 12, 2002, takriban watu 780 wameshikiliwa katika jela hiyo na hadi sasa tuhuma za kutenda uhalifu walizobambikiwa bado hazijathibitika. Kwa sasa gereza hilo la kutisha lina wafungwa zaidi ya 30.