Taathira za kisaikolojia zinazotokana na usomaji wa Qur'ani Tukufu
(last modified Fri, 21 Mar 2025 15:52:18 GMT )
Mar 21, 2025 15:52 UTC
  • Taathira za kisaikolojia zinazotokana na usomaji wa Qur'ani Tukufu

Mtaalamu mmoja wa masuala ya kifamilia amesema kuhusu taathira za kusoma Qur'ani Tukufu kwa mtazamo wa saikolojia kuwa: Kusoma maandishi ya Aya za Qur'ani na kuyazingatia kwa kina hutuliza moyo wa msomaji na hivyo kumpa somo la kujifahamu; kwa njia ambayo humfanya apate kutambua vizuri uwezo na udhaifu wake katika mazingira tofauti.

Hossein Alizadeh Kuzekanan, mtaalamu wa masuala ya familia, anasema kuhusu taathira za kisaikolojia za kusoma Qur'ani Tukufu kwa nafsi na dhati ya mwanadamu kwamba: Qur'an inaashiria kwa njia maalumu suala la tiba ya kudhikiri na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kwamba tunaweza kulifahamu vizuri suala hili kwa kusoma Aya zake takatifu. Anasema kwa mfano, tunapasa kufanya shughuli na mambo yetu kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu na kwamba kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanikiwa katika hali zote mbili za kushinda au kutofaulu kufanya jambo fulani.

Alizadeh anaongeza kuwa tunaposoma Aya za Qur'ani Tukufu kwa mazingatio, nyoyo hupata utulivu na miili pamoja na roho zetu kuwezeshwa kufuata njia na mafundisho ya Aya hizo. Hapo ndipo sisi hupata uwezo wa kudhibiti ndimi zetu, macho kutazama mambo yanayofaa, mikono kuwa safi na miguu kutembea kwenye njia nyoofu na ya haki na matokeo ya mchakato huo ni malezi ya watu wema na wenye imani safi.

Kuleta furaha na bashasha

Mtaalamu huyu wa masuala ya familia anasema kwamba kwa kutilia maanani kuwa Aya za Qur'ani Tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu ambazo ziliteremshwa kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu na kuimarisha nyoyo zao, maudhui ya Aya hizi yanawiana kikamilifu na sifa za kisaikolojia na za dhati zao. Hata wasiokuwa Waislamu wanaposikiliza Aya hizi za Mwenyezi Mungu na kuzitafakari, hukiri kwamba maneno haya huwaletea aina fulani ya matumaini, furaha na uchangamfu, ni kana kwamba yanaashiria mambo yao ya thamani yaliyopotea.

Taathira za kusoma Qur'ani

Urafiki wa pande mbili

Alizadeh anaendelea kusema kuwa: Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Maimamu watoharifu wa Nyumba yake (as) kwamba hata kuzitazama tu Aya za Qur'ani hutuliza nyoyo na kuleta usafi wa dhati. Kwa hiyo kila anayeipenda Qur'ani, Qur'ani nayo humpenda. Kwa hakika kuwa na uhusiano mzuri na Qur'ani ni kuwa na uhusiano na mambo mazuri na ya kheri, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametaja mambo mazuri na yanayomletea mwanadamu furaha ndani ya Qur'ani, na bila shaka anayeshikamana na mambo mema na ya kheri atabakia kuwa mtu mwema.

Somo la kujijua

Mwandishi huyu wa kitabu kuhusu tabia za heshima katika malezi na mafundisho ya watoto anaendelea kusema: Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'ani Tukufu amezungumzia tabia za watu kisaikolojia, kiutu, kimwili, kitabia na kidini. Kwa hivyo, mtu anayesoma Aya za Qur'ani na kuzingatia kwa kina maana zake, huwa amejifunza masomo muhimu ya kuijua nafsi yake na vile vile kupata kujua uwezo na udhaifu wake.

Hossein Alizadeh Kuzekanan, mtaalamu wa masuala ya familia anasema: Kufungamana na Qur'ani humfanya msomaji wa Aya za Mwenyezi Mungu kuwa na ujuzi wa maneno ya Qur'ani, na baada ya muda, maneno na matamshi yake huendana na mafundisho ya Qur'ani. Ujuzi wa maneno ya Qur'ani huelekeza akili na mwili wa mwanadamu katika mwelekeo huo huo, na hatimaye kufanya mienendo na tabia zake ziende sambamba na tabia za Qur'ani.

Msaada wenye nguvu wa kisaikolojia

Alizadeh anafafanua kuwa: “Moja ya athari muhimu za kisaikolojia za Qur’an ni kuwa kila mara inawalingania watu kufanya mambo mema na kusisitiza kwamba ushindi unatokana na wema na kwamba hakuna ujira wa yeyote utakaopotea bure. Habari njema hii ni msaada mkubwa wa kisaikolojia kwa watu kuendelea kufanya matendo mema.

Uwastani katika tabia

Mtaalamu huyu wa masuala ya kifamilia anasema: Tafiti zinaonyesha kwamba kuwa na uhusiano mzuri na Aya za Qura'ni Tukufu na kusoma maneno ya Mwenyezi Mungu katika kitabu hicho huibua hali nzuri ya kiroho, kuimarisha tabia, utulivu na kumshajiisha mwanadamu kuwa na tabia nzuri. Humfanya ajione akiwa mbele ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kuona haya kufanya dhambi.

Kuzuia kukata tamaa

Mwandishi huyu wa vitabu kadhaa vya malezi bora anaendelea kusema: "Magonjwa mengi ya kiakili, husuda, kiburi, kujilinganisha na wengine, kukata tamaa na kukosa matumaini huondolewa kwa kusoma Aya za Qur'ani na kupokea maadili ya Qur'ani, ambapo mtu huweza kutulia kiakili na kitabia kwa njia hiyo."

Kuunda utu salama

Anaongeza kuwa: 'Kuzifahamu sunna na taratibu za Mwenyezi Mungu na ukweli kwamba ukweli daima ni ushindi na uwongo ni wa kuharibikiwa na kutoweka, kuna taathira muhimu za kisaikolojia kwa mwanadamu. Muumini siku zote humchukulia Mwenyezi Mungu kuwa ndiye tegemeo lake kuu na anaamini kuwa yuko pamoja naye siku zote, na imani hii inayopatikana katika mafundisho ya Aya za Qur’ani, hujengeka ndani yake tabia salama njema, yenye heshima, yenye matumaini na kumfanya awe na subira katika kukabiliana na matatizo mbalimbali maishani.

Kuhamasisha utendaji

Mwalimu huyu wa elimu ya familia anamalizia kwa kusema: 'Aya za Qur'ani zinatilia mkazo uhalisia wa kivitendo wa mwanadamu, kwa sababu kuamini pekee bila kutenda hakutoshi. Ili itikadi iweze kutekelezwa kivitendo, inahitajia matendo mema. Sasa wanasaikolojia wanaamini kuwa mojawapo ya njia za kutibu wasiwasi, shinikizo la mawazo na mfadhaiko ni kutenda mambo mema.