Dec 01, 2016 12:08 UTC
  • Madai ya makosa ya kibinadamu, mbinu kuu ya kuhalalisha jinai za Marekani

Tume ya uchunguzi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imekiri rasmi kuwa ndege za kivita za nchi hiyo zilishambulia maeneo ya wanajeshi wa Syria huko Deir ez-Zor, mashariki mwa nchi hiyo.

Hatimaye Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa tume yake hiyo kuhusiana na shambulizi la anga la mwezi Septemba mwaka huu lililofanywa na ndege za muungano wa nchi zinazoongozwa na Marekani dhidi ya maeneo ya jeshi la Syria huko Deir ez-Zor. Pentagon ililazimika kuunda tume maalumu ya kuchunguza shambulio hilo baada ya Russia kukasirika mno na kutangaza wazi kuwa haiwezi kuvumilia mashambulio kama hayo.

Mkuu wa tume ya uchunguzi ya Pentagon amewaambia waandishi wa habari kuwa, shambulio hilo halikufanywa kwa makusudi na wala Marekani haikuwa na nia ya kuanzisha chokochoko mpya.  Wanajeshi wasiopungua 62 wa Syria waliuawa kwenye shambulio hilo. Inasemekana kuwa, shambulio hilo lilifanyika ili kutoa mwanya kwa magenge ya kigaidi kuishambulia na kuiteka kambi hiyo ya jeshi la Syria.

 

Taarifa za kuaminika zinaonesha kuwa, magaidi walianzisha shambulizi lao dhidi ya kambi hiyo sambamba na shambulio hilo la ndege za Marekani. Habari hizo zinaonesha kuweko mipango ya pamoja kwa namna fulani baina ya makundi ya kigaidi na muungano unaoongozwa na Marekani huko Syria kuhusu kushambuliwa kambi hiyo ya jeshi la serikali.

Hivi sasa Marekani inajaribu kujipapatua na lawama kwa kudai kuwa shambulio hilo lilifanyika kimakosa na haikuwa na nia ya kushambulia kambi ya kijeshi ya Syria. Hata hivyo ushahidi wa kuaminika unaonesha kuwa, jinai hiyo ya Wamarekani ilifanywa kwa makusudi kabisa na ni shambulio lililokuwa limepangwa tangu zamani tena kwa maelewano kamili baina ya Marekani na magenge ya kigaidi.

Kwa kweli ni jambo rahisi sana kwa Marekani kuweza kujua sehemu zilipo kambi za kijeshi za serikali na maeneo ya waasi hasa kutokana na zana za kisasa walizo nazo Wamarekani na uwezo wao mkubwa wa kijeshi kama wanavyojipigia propaganda kote ulimwenguni. Sasa kama leo hii Wamarekani wanakiri kuwa hawakujua kwamba hiyo ilikuwa ni kambi ya kijeshi, suala ambalo ni rahisi mno kulitambua katika masuala ya kijeshi, basi propaganda zote zinazoenezwa na nchi hiyo kuwa ina nguvu kubwa za kijeshi, ni uongo mtupu, na kama Wamarekani wanashindwa hata kutofautisha baina ya kambi ya kijeshi na maeneo ya magaidi, vipi wanadai kuwa wanaongoza vita vya kupambana na ugaidi? 

Wanajeshi na wananchi wa Syria wamesimama imara kuilinda nchi yao

 

Walimwengu bado hawajasahau jinai za hivi karibuni za Marekani nchini Afghanistan ambako ndege za kivita za dola hilo la kibeberu zilishambulia hospitali kwa madai ya kupambana na ugaidi na kupelekea kuuawa makumi ya wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo. Siku chache baada ya jinai hiyo, muungano unaoongozwa na Marekani ulishambulia eneo la makazi ya raia huko Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa nchini Iraq na kuua kwa umati raia 18 wakiwemo wanawake 14. Jinai nyingine za Wamarekani nchini Iraq ni kuua kwa umati wanafunzi mjini Mosul na kushambulia watu waliokuwa wamekusanyika mazikoni katika eneo la Dafuq huko Kirkuk na kuua raia 25  wakiwemo wanawake 15 na hiyo ni sehemu ndogo tu ya jinai zilizofanywa na muungano unaoongozwa na Marekani katika miezi ya hivi karibuni kwa madai ya kupambana na magaidi nchini Iraq. Amma cha kusikitisha zaidi ni kuona kuwa jinai zote hizo zinafanyika huku Umoja wa Mataifa ukiendelea kukaa kimya bila ya hata kufumbua mdomo wake kulaani jinai hizo. 

Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, lengo la Marekani ni kuidhoofisha serikali ya Syria na kuyatia nguvu magenge ya kigaidi, na kila inapoona magenge hayo yameelemewa na yanakaribia kusambaratishwa, Wamarekani huzuka na mbinu za kila namna kama kushinikiza usimamishaji vita, kukimbilia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kushambulia maeneo ya jeshi la Syria na halafu kudai kuwa jinai zake hizo zimefanyika kimakosa.

Tags