Mwislamu mwingine auawa Marekani kutokana na chuki za kidini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21274-mwislamu_mwingine_auawa_marekani_kutokana_na_chuki_za_kidini
Habari kutoka jimbo la California nchini Marekani zinasema kuwa raia mmoja wa nchi hiyo wa dini ya Kiislamu ameuawa nje ya msikiti katika tukio jingine linalodhihirisha chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 12, 2016 08:13 UTC
  • Mwislamu mwingine auawa Marekani kutokana na chuki za kidini

Habari kutoka jimbo la California nchini Marekani zinasema kuwa raia mmoja wa nchi hiyo wa dini ya Kiislamu ameuawa nje ya msikiti katika tukio jingine linalodhihirisha chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Sajenti wa Polisi katika jimbo hilo Adam Darough amethibitisha kutokea mauaji hayo na kubainisha kuwa, raia mmoja wa Marekani mwenye chuki dhidi ya Uislamu alianzisha ugomvi na kisha kumdunga kisu muumini huyo alipokuwa akitoka msikitini karibu na kituo cha Kiislamu cha Jamiaa Raazi Islamic Center, eneo la Simi Valley jimboni California siku ya Jumamosi. Kwa mujibu wa afisa huyo wa polisi, mtu huyo anayetambulika kama John Matteson, ana historia ya kuwashambulia Waislamu nchini Marekani.    

Chuki dhidi ya Uislamu Marekani

Uchunguzi uliofanywa katika majimbo 20 ya Marekani na kwenye mji wa New York ambapo matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kukabidhiwa kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Uhalifu katika jamii ya Marekani unaonesha kuwa, uhalifu unaotokana na chuki umeongezeka kwa karibu asilimia sita nchini Marekani, lakini vitendo vya kihalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka kwa asilimia 89. 

Baada ya kutokea shambulizi la mjini San Bernardino huko California, Donald Trump aliitaka serikali ya Marekani iwapige marufuku Waislamu kuingia nchini humo. Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu limetangaza kuwa, viteondo vya kihalifu dhidi ya Waislamu vimeongezeka sana baada ya tukio hilo la Septemba 2, 2015.

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, mwenye chuki dhidi ya Uislamu

Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka huu, Kituo cha Kiislamu katika jimbo la Florida Marekani kiliteketezwa moto na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu. Baada ya hapo Masjidul Karim wa mji wa Providence huko Rhode Island nchini Marekani ulitumiwa barua yenye chuki za kidini dhidi ya Waislamu. Miongoni mwa maneno yaliyokuwemo kwenye barua hiyo yanasema: Donald Trump, rais mteule wa Marekani atawatendea maovu Waislamu kuliko vile Hitler alivyowatendea Mayahudi.