Washington Post: Marekani inajitayarisha kuishambulia Korea ya Kaskazini
Gazeti moja linalochapishwa nchini Marekani limeandika kuwa Marekani na Korea ya Kusini zinafanya mazoezi katika maneva yao pamoja kwa ajili ya kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Korea ya Kaskazini.
Shirika la Habari la Tasnim limenukuu toleo la leo la gazeti la Washington Post ambalo limeandika kuwa: Marekani na Korea ya Kusini leo zimeanza maneva makubwa ya kijeshi ya pamoja, ambapo moja ya sehemu ya maneva hivyo imetajwa kuwa ni kwa ajili ya kujiandaa nchi hizo kufanya mashambulizi yatakayolenga kwa usahihi vituo muhimu vya makombora na nyuklia vya Korea ya Kaskazini.
Maneva hayo siku zote yamekuwa yakikabiliwa na radiamali kali ya Pyongyang, hata hivyo matamshi yaliyotolewa ndani ya Korea ya Kaskazini kwenyewe dhidi ya maneva hiyo ya mwaka huu ya nchi mbili hizo ni makali mno zaidi. Marekani na Korea ya Kusini zimetuhumiwa kuwa zinafanya njama ili kutekeleza oparesheni ya kuupindua utawala wa Kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un.