Korea Kaskazini yaonyesha kombora jipya la balestiki la SLBMs
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27798-korea_kaskazini_yaonyesha_kombora_jipya_la_balestiki_la_slbms
Katika hali ambayo taharuki imetanda katika Peninsula ya Korea , serikali ya Korea Kaskazini imezindua kombora lake jipya la balestiki la nyambizi (SLBMs).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 15, 2017 07:49 UTC
  • Korea Kaskazini yaonyesha kombora jipya la balestiki la SLBMs

Katika hali ambayo taharuki imetanda katika Peninsula ya Korea , serikali ya Korea Kaskazini imezindua kombora lake jipya la balestiki la nyambizi (SLBMs).

Kanali ya televisheni ya taifa imeonysha kombora hilo la balestiki linaloitwa Pukkuksong-2 SLBMs pamoja na makombora mengine ya wastani ya KN-08 na KN-14 katika Medani ya Kim Il Sung katika mji mkuu Pyongyang.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jung-un ameongoza uzinduzi huo leo Jumamosi, siku ambayo taifa hilo linaadhimisha miaka 105 tangu kuzaliwa kwa muasisi wa nchi hiyo, Kim Il Sung, ambaye ni babu yake.

Hii ni mara ya kwanza kwa Korea Kaskazini kuonyesha hadharani kombora lake lenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 1000.   

Kombora jipya la balestiki la Korea Kaskazini

Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesema kuwa, siasa za Donald Trump, Rais wa Marekani kuihusu nchi hiyo ni za kihujuma na za shari zaidi kuliko zile za mtangulizi wake Barack Obama.

Han Song Ryol, amesema kuwa, matamshi yanayotolewa na rais huyo wa Marekani mara zote ni yenye vitisho na kwamba Pyongyang imejiandaa kukabiliana na hatua zozote za kichokozi za Washington. 

Haya yanajiri wiki moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini kutangaza kwamba Pyongyang imelifanyia majaribio kombora jipya la balestiki la kilomita 800 kwa mafanikio makubwa, siku moja baada ya jeshi la Korea Kaskazini kulifanyia majaribio kombora jipya la balestiki katika pwani ya mashariki mwa nchi hiyo kwenda maji ya upande wa Korea Kusini.