Apr 18, 2017 15:33 UTC
  • HRW yalaani shambulizi la Marekani dhidi ya msikiti nchini Syria

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani shambulizi la anga la Marekani dhidi ya msikiti mmoja nchini Syria mwezi uliopita, ambapo makumi ya watu waliuawa.

Ole Solvang, Mtafiti Mkuu wa Human Rights Watch amesema uchunguzi wao umebaini kuwa, Marekani ilishindwa kuchukua hatua za tahadhari kabla ya kutekeleza shambulizi hilo.

Amesema madai ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kwamba picha zake za satalaiti zilishindwa kubaini iwapo jengo walilolishambulia lilikua msikiti au ngome ya kundi la kigaidi la al-Qaida hayaingii akilini.

Afisa huyo wa Human Rights Watch amesema uchunguzi wao umebainisha kuwa, jeshi la anga la Marekani liliwalenga raia waliokuwa wakitoroka msikitini hapo baada ya hujuma hiyo kwa makombora ya "Hellfire".

Msikiti ulioshambuliwa na US huko Syria

Machi 16, raia wasiopungua 46 waliuawa katika shambulio hilo la anga la US lililolenga Msikiti wa Umar Ibn Al-Khaṭṭab uliokuwa umejaa waumini ndani yake karibu na mji wa Halab kaskazini mwa Syria. Watu wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa katika shambulio hilo lililofanywa katika kijiji cha al-Jineh kilichopo kilomita 30 magharibi mwa mji wa Halab. 

Jamhuri ya Kiislamu kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Bahram Qassemi ililaani hujuma hiyo na kusema kuwa: "Kushambulia maeneo matukufu na ya kidini kwa lengo lolote lile ni jambo linalolaaniwa na haliwezi kutetewa hata kidogo."

Tags