Macron aahidi kufungua ukurasa mpya katika siasa za Ufaransa
Mgombea wa urais wa harakati ya mrengo wa wastani wa En Marche nchini Ufaransa ameahidi kubadili taswira na mkondo wa siasa za nchi hiyo iwapo ataibuka mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo.
Emanuel Macron ametoa ahadi hiyo baada ya kushinda duru ya kwanza akiwa pamoja na mwanasiasa wa mrengo wa kulia, Marine Le Pen na kuongeza kuwa, amewataka wananchi kumuunga mkono kukabiliana na kile anachoitaja kama tishio kwa utaifa akisistiza kuwa kuna haja ya kuufanyia marekebisho mfumo wa siasa za nchi hiyo ya Ulaya.
Macron aliibuka mshindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Ufaransa hapo jana kwa kupata asilimia 23.7 ya kura, akifuatiwa na Marine Le Pen aliyepata asilimia 21.5, kulingana na matokeo ya mwisho ya Tume ya Uchaguzi.
Rais wa Ufaransa François Hollande na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamepongeza Emmanuel Macron kwa ushindi huo kwa njia ya simu huku mgombea aliyembwagwa wa Chama cha Kisoshalishti, Benoit Hamon, Waziri Mkuu wa chama hicho Bernard Cazeneuve, na mgombea wa Chama cha Mrengo wa Kulia, Francois Fillon wote wakitoa wito kwa wafuasi wao kumuunga mkono Macron katika duru ya pili ya uchaguzi huo.
Siku chache kabla ya kuanza uchaguzi huo, Pierre Moscovici, Kamishna wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Umoja wa Ulaya alisema EU haijajiandaa na senario ya Marine Le Pen kutoka mrengo wa kulia wenye misimamo mikali kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Ufaransa na bila ya shaka taasisi hiyo inakaribisha kuwepo Ufaransa imara katika Ulaya imara na yenye nguvu.
Duru ya pili ya uchaguzi huo wa urais wa Ufaransa inatazamiwa kufanyika tarehe 7 ya mwezi ujao wa Mei, huku Macron akitazamiwa kuibuka mshindi kwa asilimia 64, kwa mujibu wa tafiti za maoni za hivi punde.