Waislamu Ufaransa watahadharishwa kuhusu ongezeko la mashambulizi ya kigaidi
Viongozi wa makundi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu nchini Ufaransa wamewatahadharisha wafuasi wa dini hiyo kuhusu uwezekano wa kuongezeka mashambulizi yanayowalenga Waislamu nchini humo.
Viongozi hao ambao wamelaani shambulizi lililofanyika usiku wa kuamkia leo karibu na Msikiti wa Arrahma eneo la Avignon kusini mwa Ufaransa, wamewataka Waislamu nchini humo kuwa macho zaidi.
Viongozi wa jumuiya za Kiislamu Ufaransa pia wamewataka maafisa wa serikali ya Paris kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulizi hilo na kuzidisha ulinzi kandokando ya vituo vya kidini.
Watu 8 wamejeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na watu wawili wasiojulikana dhidi ya watu waliokuwa wamemaliza ibada ya Swala karibu na Msikiti wa Arrahma eneo la Avignon.
Wito wa viongozi wa Kiislamu nchini Ufaransa umetolewa baada ya mwendesha mashtaka wa eneo la Avignon kudai kuwa, shambulizi lililolenga Waislamu karibu na msikiti huo halikuwa la kigaidi.
Shambulizi la kulengwa Waisalmu kwa risasi huko Avignon limeibua wasiwasi miongoni mwa Waislamu Ufaransa ambao hivi karibuni walishuhudia mtu moja akijaribu kuwakanyaga Waislamu kwa gari nje ya msikiti mmoja kusini mashariki mwa Paris.