NATO yaunga mkono stratejia mpya ya Marekani kuhusu Afghanistan
Muungano wa Kijeshi wa NATO umeunga mkono uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuongeza wanajeshi wengine nchini Afghanistan katika kalibu ya stratejia mpya ya Washington.
Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Nato ameunga mkono stratejia hiyo mpya ya ikulu ya Marekani (White House) kuhusu Afghanistan na kueleza kuwa nchi 15 wanachama wa muungano huo pia zimeonyesha azma yake ya kutuma wanajeshi zaidi huko Afghanistan.
Uingereza ambayo ni nchi mwanachama wa Muungano wa Nato pia imekaribisha stratejia hiyo mpya ya Marekani kuhusu Afghanistan.
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye mwaka jana aliingia madarakani kwa kutoa ahadi ya kuwarejesha nyumbani haraka wanajeshi wa nchi hiyo waliopo Afghanistan, juzi alibadili msimamo wake huo na kuzungumzia nia yake eti ya kuzidisha oparesheni za kijeshi dhidi ya kundi la Taliban nchini humo. Katika mkakati wake huo mpya kuhusu Afghanistan, Rais Trump ameamuru kutumwa wanajeshi wengine elfu nne wa nchi hiyo ili kujiunga na wenzao elfu nane na 400 waliopo nchini humo.