Marekani kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na Myanmar inayoua Waislamu
Katika hali ambayo jamii ya kimataifa inaendelea kulaani na kukosoa vikali mauaji na ukatili wanaofanyiwa Waislamu wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, Marekani ipo mbioni kuimarisha ushirikiano wake wa kijeshi na nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Kongresi ya Marekani inatazamiwa kujadili muswada wa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi wa US na Myanmar, huku watawala wa Washington wakiendelea kufumbia macho jinai dhidi ya Waislamu hao wa Kirohingya.
Walter Lohman, Mkurugenzi wa Mipango barani Asia wa shirika la kutetea haki za binadamu la Heritage Foundation amekosoa vikali muswada huo akisisitiza kuwa: "Kuimarisha uhusiano wa moja kwa moja wa kijeshi na Burma wakati huu ni jambo ambalo haliingii akilini, hatua hiyo inatuma ujumbe wa kuogofya kwa dunia."
Hii ni katika hali ambayo, nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeendelea kulaani mauaji na jinai wanazofanyiwa Waislamu hao wa kabila la Rohingya.
Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wanaokutana katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana wanatazamiwa kujadili wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la Myanmar likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali, dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine tokeo Agosti 25.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Baraza la Ulaya lilitoa wito wa kukomeshwa mauaji hayo ya kimbari yanayofanywa na mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchi hiyo.
Hayo yanajiri huku Umoja wa Mataifa ukiwa umeshatangaza katika ripoti zake mbalimbali kwamba, kumekuwa kukifanyika mateso na vitendo vya kinyama dhidi ya Waislamju wa Myanmar.