UNHCR: Misaada zaidi inahitajika kwa ajili ya Waislamu Warohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34877-unhcr_misaada_zaidi_inahitajika_kwa_ajili_ya_waislamu_warohingya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza mara mbili juhudi za kuwasaidia wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia mauaji ya umati Myanmar na kupata hifadhi nchini Bangladesh.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 26, 2017 16:01 UTC
  • UNHCR: Misaada zaidi inahitajika kwa ajili ya Waislamu Warohingya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuongeza mara mbili juhudi za kuwasaidia wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia mauaji ya umati Myanmar na kupata hifadhi nchini Bangladesh.

Wito huo umekuja wakati kukiwa na hofu kwamba hali ya wakimbizi 436,000 walioingia Bangladesh kutoka Myanmar mwezi uliopita inaweza kuwa mbaya. UNHCR imeendelea kupeleka misaada kwa njia ya anga lakini bado haitoshelezi mahitaji ya wakimbizi hao. Adrian Edward msemaji wa UNHCE Geneva amesema, "Licha ya juhudi zinazofanyika huko, wimbi kubwa la watu wanaosaka usalama linazidi uwezo wa huduma, na hali ya wakimbizi hawa bado haijatengamaa. Wengi wa waliowasili hivi karibuni wameathirika sana kisaikolojia, licha ya kupata hifadhi Bangladesh na bado wanakabiliwa na hali ngumu."

UNHCR na washirika wengine wa kimataifa wa misaada wanaendelea kuwasaidia wakimbizi hao hususani wasiojiweza kama watoto, wanawake, walemavu na wazee wanaohitaji msaada wa haraka wa malazi, chakula, maji na huduma za afya.

Waislamu wa jamii ya Rohingya wakiomba misaada

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya nchi zilizo mstari wa mbele kutuma misaada ya dharura kwa Waislamu wa Rohingya. Katika kipindi cha wiki mbili Iran imetuma ndege mbili za mizigo zilizobeba shehena za misaada kwa ajili ya Waislamu Warohingya walioko katika kambi za wakimbizi Bangladesh.

Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu ambapo tokea wakati huo Waislamu zaidi ya elfu sita wameuawa katika hujuma ya jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.