Mashirika ya kutetea haki za binadamu Marekani yampeleka Trump kotini
Mashirika ya kutetea haki za binadamu katika jimbo la Maryland nchini Marekani yameenda mahakamani kuushtaki utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo juu ya marufuku mpya iliyo dhidi ya wahajiri.
Asasi hizo za kiraia chini mwavuli wa muungano wa American Civil Liberties Union (ACLU) zimesema marufuku mpya iliyotangazwa na Trump Jumapili iliyopita ni kinyume cha sheria na ni hatua inayokiuka haki za binadamu.
Anthony Romero, Mkurugenzi Mkuu wa ACLU ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Marufuku hii mpya inasalia kuwa marufuku dhidi ya Waislamu na kinyume cha sheria kuwabagua watu kwa misingi ya utaifa au dini yao."
Hivi karibuni, Rais Donald Trump aliziongeza Korea Kaskazini, Chad na Venezuela katika orodha ya nchi ambazo raia wao hawaruhusiwi kufanya safari nchini Marekani, kwa kisingizio cha kulinda usalama wa taifa.
Nchi nyingine ni Iran, Syria, Libya, Somalia na Yemen, huku Sudan iliyokuwa katika orodha ya awali ikiondolewa katika orodha mpya.
Kamisheni ya Umoja wa Afrika na baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa zimekosoa vikali marufuku hiyo iliyo dhidi ya uhajiri ya Trump.