Watu 58 wauawa katika hujuma ya kigaidi Las Vegas, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35139-watu_58_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_las_vegas_marekani
Watu 58 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa katika mji wa Las Vegas nchini Marekani ambayo imetajwa kuwa tukio mbaya zaidi la ufyatuaji risasi kiholela nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2017 10:55 UTC
  • Watu 58 wauawa katika hujuma ya kigaidi Las Vegas, Marekani

Watu 58 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa katika mji wa Las Vegas nchini Marekani ambayo imetajwa kuwa tukio mbaya zaidi la ufyatuaji risasi kiholela nchini humo.

Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa,  hujuma hiyo ilitokea mapema Jumatatu asubuhi karibu na eneo maarufu la wacheza kamari la Mandalay Bay katika mji wa anasa wa Las Vegas na kwamba hadi sasa watu wasiopungua 58 wamethibitishwa kuuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa. Gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo ametajwa kuwa Stephen Paddock aliyekuwa na umri wa miaka 64. Imedokezwa kuwa alikuwa amechukua chumba cha ghorofa ya 32 katika hoteli na kisha akaanza kuwamimiminia risasi watu waliokusanyika katika tamasha la muziki. Baadhi ya taarifa zinasema Paddock alijiua kabla ya polisi kuvunja mlango wa chumba chake huku baadhi ya ripoti zikisema maafisa wa polisi ndio waliompiga risasi na kumuua na kwamba katika chumba chake kulipatikana bunduki zingine 10 ambazo zilikuwa bado hazijatumika.

Maafisa wa polisi Las Vegas wakati wa tukio la ugaidi

Kumeibuka mjadala nchini Marekani baada ya mkuu wa Polisi Las Vegas Sheriff Joseph Lombardo kusema tukio hilo si la kigaidi akidai kuwa uchunguzi bado unaendelea kubaini lengo la hujuma hiyo.

Hii ni katika hali ambayo sheria ya jimbo la Las Vegas inataja ugaidi kuwa ni kutumia au kujaribu kutumia mabavu kusababisha madhara au kifo kwa watu wengine.