HRW: Jeshi la Myanmar linawaua na kuwanajisi Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35247-hrw_jeshi_la_myanmar_linawaua_na_kuwanajisi_waislamu_wa_myanmar
Shirika la kutetea haki za binadmau la Human Rights Watch (HRW) limesema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 05, 2017 07:56 UTC
  • HRW: Jeshi la Myanmar linawaua na kuwanajisi Waislamu wa Myanmar

Shirika la kutetea haki za binadmau la Human Rights Watch (HRW) limesema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatano na HRW, katika tukio moja la Agosti 27, Jeshi la Myanmar lilivamia eneo ambalo wanakijiji wengi Waislamu walikuwa wamekimbilia kwa hofu ya kushambuliwa na kuuawa. Wanajeshi walipofika hapo waliwafyatulia risasi kiholela Waislamu, huku wakiwanajisi wanawake na kuwadunga wengine visu.

Naibu Mkurugenzi wa HRW barani Asia Phil Robertson amesema jinai zinazotekelezwa na Myanmar hazipaswi kulaaniwa tu kwa maneno bali dunia inapaswa kuchukua hatua za kivitendo kukabiliana na hali hiyo. Amesema picha za satalaiti zinaonyesha kijiji hicho kiliteketezwa kabisa baada ya tukio hilo huku miili ya Waislamu zaidi ya mia moja waliouawa ikipakiwa katika malori ya kijeshi na kupelekwa kusikojulikana.

Waislamu wa Myanmar wakikimbilia usalama baada ya vijiji vyao kuteketezwa na jesh la nchi hiyo

Hayo yanajiri wakati mashirika ya kimataifa yasiyo ya serikali yanasema kuwa hatua za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai za wazi dhidi ya binaadamu ambapo sambamba na kulaani jinai hizo yameitaka dunia kukabiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuzuia hali hiyo.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa. Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya nusu milioni kati yao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.